NEWS

Tuesday 24 October 2023

Mpango wa ujenzi uwanja wa ndege Mugumu wakwama kwa miaka 18



Sehemu ya mji wa Mugumu
--------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Mugumu
-----------------------------------------------


MPANGO wa kujenga uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, Mara umekwama kwa miaka takriban 18 sasa. 

Taarifa zilizopo zinaonesha mpango wa kujenga uwanja huo ulianza mwaka 2005 ambapo Tathmini ya Athari za Kimazingira (Enviromental Impact Assessment - EIA) na maandalizi mengi yalianza chini ya ufadhili wa mwekezaji wa kampuni ya Grumeti. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mwekazaji huyo alitumia zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwenye malipo mbalimbali, ikiwemo fidia kwa wananchi waliotakiwa kupisha eneo la mradi huo na kuhamisha Shule ya Msingi ya Serikali ya Burunga. 

Lengo la mpango huo lilikuwa ni kuufanya mji wa Mugumu kuwa kitovu cha utalii. 

Taarifa zinasema ujenzi wa uwanja huo ungejengwa kwa miezi 30 na kisha kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya uendeshaji. 

Hata hivyo, alipouliza na Sauti ya Mara mjini Mugumu juzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Makuruma alisema hakuna mkataba wowote baina ya hamashauri hiyo na mwekezaji huyo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo. 

“Iko hivi mkataba haupo, na kampuni ya Grumeti ilikuwa inafanya tu facilitation (uwezeshaji), hata hiyo shilingi bilioni 1.1 walitoa tu kuonesha nia njema,” alifafanua Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kupitia chama tawala - CCM. 

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti inachofanya kwa sasa ni kutafuta wawekezaji ambao wanaweza kuungana nayo kujenga mradi huo. 

Katika miaka ya hivi karibuni, wafanyabishara wa mji wa Mugumu walionesha kiu ya kuunga mkono ujenzi wa uwanja huo, baada ya kuona unachelewa na kuanzisha kundi la WhatsApp kwa ajili ya kuchangia mafuta ya kuanza kazi, lakini inaelezwa kuwa hakuna hata senti moja iliyochangwa hadi sasa. 

“Hakuna fedha cash (taslimu) zilizochangwa ila wafanyabiashara tuliaahdi kuchangia mafuta lakini baada ya kuona wahisani wakubwa wamerudi nyuma na sisi tukarudi nyuma,” Mwenyekiti wa kundi hilo la wafanyabisahara wa Mugumu aliiambia Sauti ya Mara kwa njia ya simu. 

Aliongeza: “Vibali vyote vipo hata vya mazingira, na uwanja huu ungejenwa ungeubadilisha sana mji wetu wa Mugumu.” 

Ujenzi wa uwanja huo ungeweza kutengeneza fursa lukiki za kiuchumi, zikiwemo ajira kwa vijana wa wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kwa ujumla. 

Inaelezwa kuwa ujenzi wa uwanja huo ulibuniwa kuwa wa kisasa ukiwa na hudumu zote muhimu kama ilivyo kwenye viwanja vingi vya ndege vya kimataifa. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages