NEWS

Monday 23 October 2023

Rais Samia: Mikataba yetu na DP World imezingatia maoni ya Watanzania
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------


RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan (pichani juu kushoto), amesema mikataba mitatu ya uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam iliyosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai, imezingatia maoni ya makundi mbalimbali ya Watanzania, sheria na taratibu zote za nchi. 

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba hiyo kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali na Kampuni ya DP World, iliyofanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma, jana Jumapili. 

Rais Samia alifafanua kuwa Serikali ilisikiliza maoni mbalimbali yaliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, viongozi wa dini na baadhi ya viongozi wastaafu nchini. 

Alisema mikataba iliyosainiwa imetokana na makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Tanzania na Mamlaka ya Dubai ambao wameridhia mahitaji na matakwa ya nchi kama yalivyoainishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa. 

Mikataba iliyosainiwa ni Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement), Mkataba wa Upangishaji Ardhi (Lease Agreement) na Mkataba wa Uendeshaji wa Bandari (Concession Agreement). 

Rais Samia alisema uimarishwaji utakaofanywa kupitia uwekezaji huo utakuza biashara za ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani, na hivyo kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa Taifa. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages