NEWS

Wednesday 11 October 2023

Operesheni maalum ilivyofichua kilimo cha bangi na viwanda vyake Bonde la Mto Mara



Sehemu ya mafurushi ya bangi iliyokamatwa katika Bonde la Mto Mara
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
-----------------------------
 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) nchini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Akiba (Mgambo) na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum dhidi ya kilimo cha bangi katika Bonde la Mto Mara. 

Operesheni hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na kufanikisha uchomaji wa ekari 807 za mashamba ya bangi, ukamataji wa magunia 507 ya bangi kavu iliyo tayari kusafirishwa, magunia 50 ya mbegu za bangi, watuhumiwa 11 na uteketezaji wa viwanda viwili vidogo vilivyokuwa vikitumika kuchakata na kufungasha zao hilo haramu. 


Baadhi ya magunia ya bangi yaliyokamatwa kiwandani katika Bonde la Mto Mara

Akizungumzia wakati wa operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA nchini, Aretas Lyimo baadhi ya wakazi wa Bonde la Mto Mara walilibadilisha eneo hilo kuwa la kilimo cha bangi, huku wakitishia kumdhuru yoyote atakayeingia huko bila ridhaa yao. 

“Kitendo kinachofanywa na wananchi waliopo katika eneo la mto Mara ni kinyume na sheria, viongozi wa serikali na wananchi ambao sio wakazi wa hapa hawaruhusiwi kabisa kuingia eneo la bonde. Uwepo wa daraja lililopo katika mojawapo ya vijito vinavyopeleka maji mto Mara linatumika kama kizuizi cha watu kwenda kwenye hifadhi ya bonde la mto inakolimwa bangi. Ili mtu avuke anatakiwa kujieleza nia na madhumuni ya kuvuka kuelekea upande wa pili, na wahusika wasiporidhika na maelezo hawakuruhusu kuendelea na safari,” alisema Lyimo. 

Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyopakana na bonde hilo pamoja na wananchi waliojimilikisha Bonde la Mto Mara ambalo ni muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na uchumi wa taifa, wamekuwa wakikodisha na kuuza mashamba ya kulima bangi ndani ya hifadhi ya bonde hilo. 


Kamishna Jenerali wa DCEA nchini, Aretas Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo aliomba wizara husika kushirikiana na vyombo vya dola kutokomeza kilimo cha bangi katika bonde hilo kwani bado mashamba ya bangi ni mengi pembezoni mwa mto Mara na maji yake yanatumiwa unaotumiwa kumwagilia. 

“Tukiacha kilimo cha bangi kiendelee na kuwaacha wananchi waendelee kuchepusha maji ya mto kumwagilia bangi mwisho wa siku itaharibu ikolojia katika mbuga ya Serengeti na mto kwa ujumla. Ni vema tukashirikiana kuhakikisha eneo hili linasimamiwa vema ili kusitisha kilimo cha bangi,” alisisitiza Lyimo. 
Bangi ikiteketezwa kwa moto katika Bonde la Mto Mara

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages