NEWS

Thursday 12 October 2023

Right to Play, AICT waadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike wakitetea haki yake ya kupata elimu



Washindi wakikabidhiwa kombe wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike katika Shule ya Msingi Nyansangero iliyopo kata ya Nyamwaga wilayani Tarime, Mara.
-------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime –
Mara Online News
-----------------------------


SHIRIKA la Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, limetumia maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike kutetea haki ya kupata elimu na kukemea vitendo vya ukatili kwa watoto. 

Maadhimisho hayo yalifanyika jana Jumatano kupitia bonanza la michezo na burudani kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyansangero iliyopo kijiji cha Komarera katika kata ya Nyamwaga wilayani Tarime, Mara. 





Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na pete, kukimbia wakiwa na chupa kichwani, pia burudani kama vile ngonjera, nyimbo na maigizo yenye ujumbe wa kumlinda mtoto wa kike na umuhimu wa kumpatia elimu, ambapo washindi walizawadiwa kombe na zawadi nyingine.

Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alitumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii kuwapa watoto wa kike thamani sawa na wa kiume, lakini pia kuwapunguzia majukumu ya kifamilia. 

“Tuwapunguzie watoto wa kike majukumu na tuwape thamani na fursa sawa na watoto wa kiume, Mungu aliwaumba wakiwa na thamani sawa, harakati zilizopo ni kuonesha kuwa watoto wa kike na kiume wote wana haki ya kuendelezwa kielimu waweze kutimiza ndoto zao,” alisema Rebeca. 
Rebeca Bugota akizungumza katika maadhimisho hayo

Naye Katekista wa Kanisa Katoliki (RC) la Nyamwaga, Bernard Mariba alitumia nafasi hiyo kutoa wito wa kuhamasisha wazazi kujitokeza kwa wingi katika harakati zinazofanyika kutetea haki za mtoto wa kike na kuweka kwenye vitendo yale yote wanayojifunza na kusikia. 

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Mradi wa Kukuza Ubora wa Elimu na Elimu Jumuishi, chini ya usimamizi wa Right to Play na AICT, kwa lengo kuu la kumtetea na kumlinda mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na mila kandamizi, hususan katika nyanja ya elimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages