NEWS

Monday 2 October 2023

Rais wa Barrick aomba juhudi za pamoja kumaliza uvamizi mgodi wa North Mara



Rais na CEO wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano na viongozi wa serikali na kijamii uliofanyika kwenye Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Ijumaa iliyopita.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Nyamongo
-----------------------------------------------


RAIS na Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow ameomba juhudi za pamoja zifanyike kukomesha uvamizi unaofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama ‘intruders’ katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara. 

Bristow alitoa kauli hiyo Ijumaa iliyopita, akielekeza ombi hilo kwa viongozi wa serikali na jamii inayozunguka mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara. 

“Kama ambavyo nimekuwa nikipokea maombi yenu mengi na kuyatekeleza, na mimi nina ombi moja kwenu; ombi langu nikwa kila mmoja wetu kwamba tufanye kazi kwa pamoja kutokomeza hii tabia (uvamizi mgodini),” Bristow alisema katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na viongozi hao, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele. 

Alikuwa akihitimisha taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu utendaji wa migodi ya Barrick nchini, North Mara na Bulyhanhulu uliopo wilayani Kahama, Shinyanga. 

Mbali na mafanikio ambayo Barrick imeendelea kuyapata tangu mwaka 2019, Bristow alisema vitendo vya uvamizi katika mgodi wa North Mara havikubaliki. 

Rais na CEO huyo wa Barrick alionekana kushangazwa na vitendo hivyo kuendelea kufanywa na vijana na watu wazima katika sehemu ya Tanzania ambayo ni nchi yenye amani. 

“Tanzania sio nchi ya vurugu, najua tunalijua tatizo na tunaweza kulimaliza,” alisema Bristow akifananisha uvamizi huo na alichokiita ‘dark issue’. 

Baadaye katika hutuba yake, DC Mntenjele alimhakikishia kiongozi huyo wa Barrick kuwa juhudi kubwa zitafanyika kukomesha uvamizi huo. 

“Uvamizi mgodini ni jambo ambalo hatupendezwi nalo. Tutafanya mikutano ya kuelimisha vijana kuachana na vitendo hivi ili wajihushe kwenye shughuli mbadala kama kilimo badala ya kutegemea uvamizi mgodini,” alifafanua. 


Sehemu ya viongozi wa serikali na kijamii mkutanoni

Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, DC Mntenjele alisema sio kwamba limeshindwa kutumia nguvu kubwa kudhibiti wavamizi hao, bali suala la haki za binadamu pia lazima lizingatiwe kwa maslahi mapana ya uwekezaji huo. 

“Sio kwamba tumeshindwa lakini suala la haki za binadamu ni la muhimu. Tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha uvamizi huu unaisha,” alisema DC huyo. 

Alitolea mfano wa mradi wa kilimo-biashara ulioanzishwa na Kampuni ya Barrick katika kijiji cha Matongo kama moja ya miradi inayoweza kusaidia vijana kupata kipato, baada ya kuvamia mgodi wa North Mara kwa ajili ya kuiba mawe ya dhahabu. 

“Tutafanya mikutano kuhamasisha vijana kufanya shughuli halali za kujipatia kipato,” alisisitiza. 

Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Amini Msuya alisema vijana wanaovamiwa mgodi huo wanatumiwa na wafanyabiashara ya dhahabu na kwamba serikali imejipanga kufanya kila linalowezekana kuwadhibiti. 

“Vijana wanatumwa kuingia mgodini, tutawadhibiti wanaowatuma,” alisema Mhandisi Msuya. 

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alisema mgodi wa North Mara umefanya maendeleo makubwa katika jimbo hilo, hivyo lazima juhudi zifanyike kuyalinda mafanikio hayo. 

Kwa mujibu wa Waitara, vijana wanaovamia mgodi huo wanatoka katika maeneo mbalimbali na sio vijiji vilivyo jirani na mgodi huo pekee. 

“Tutalinda mafanikio ambayo tumeyapata mgodini kwa kuondoa uvamizi mgodini,” Mbunge huyo alisema. 

Hata hivyo , Rais na CEO wa Barrick, Bristow, alionekana kufarijika baada ya kusikia kuwa viongozi wa serikali na kijamii wanatambua uwepo wa tatizo la uvamizi huo. 

Awali, Bristow alieleza katika taarifa yake kuwa Barrick imewekeza shilingi karibu trilioni 7.5 katika uchumi wa Tanzania tangu mwaka 2019 ilipoanza kuendesha migodi ya North Mara na Bulyanhulu kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga. 

Alisema kampuni ya Barrick ambayo imeajiri watu zaidi ya 5,000 pia imebaki kuwa mlipa kodi mkubwa nchini Tanzania, huku akitabiri matokeo chanya zaidi katika miaka ijayo. 

Bristow alisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa ajira kwa Watanzania, hususan katika maeneo yaliyo jirani na migodi yake, huku wanawake wakipewa pia fursa maalumu. 

“Bado tunaendelea kuwekeza kwenye migodi ya North Mara na Bulyanhulu, na bado tunaweza kufanya zaidi katika miaka ijayo,” alisema Bristow ambaye aliambatana na Meneja Mkazi wa Barrick Tanzania - Utawala na Fedha, Dkt Melkiory Ngido katika mkutano huo. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages