NEWS

Monday 2 October 2023

Tarime DC yatumia milioni 500 za mapato ya ndani kujenga kituo cha afya Kwihancha, kuhudumia wananchi 16,000



Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho akiongoza wajumbe wa kamati hiyo kukagua sehemu ya ndani katika mojawapo ya majengo ya Kituo cha Afya Kwihancha, hivi karibuni.
------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------


HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) imeweka historia mpya baada ya kutumia shilingi milioni 600 zilizotokana na mapato yake ya ndani, kugharimia ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata ya Kwihancha, kilomita chache kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti. 

Kituo hicho kitahudumia wananchi zaidi ya 16,000 kutoka vijiji vyote vinavyounda kata ya Kwihancha na hata baadhi ya vijiji vya kata jirani. 

Vijiji vya kata Kwihancha ambavyo vitanufaika na kituo hicho ni Kwihancha, Gibasso, Karakatonga na Nyabirongo. 

Aidha, kituo hicho kitanufaisha baadhi ya vijiji vya kata jirani za Gorong’a na Kemambo; ambavyo ni Masurura, Kitawasi na Murito. 

Kijiografia kituo hicho cha afya kipo katika eneo zuri la kutoa huduma za matibabu hata kwa wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) waliopo eneo la Lamai ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. 

Taarifa zinasema huo ndio mradi wa kwanza mkubwa ambao umetekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kutumia mapato ya ndani. 

Makusanyo ya halmashauri hiyo yamepaa hadi shilingi bilioni 9.22 sawa na asilimia 116 ya lengo lake kwa mwaka wa fedha 2022/2023. 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho anasema wananchi wa kata ya Kwihancha wamepokea mradi huo wa kituo cha afya kwa furaha kubwa. 

“Mradi wa Kituo cha Afya Kwihancha upo vizuri sana na wananchi wamefurahi kuona CCM inavyowajali,” Ngicho aliliambia gazeti hili muda mfupi baada ya kuongoza Kamati ya Siasa ya Wilaya chama hicho tawala kutembelea mradi huo, wiki iliyopita. 

Sehemu ya majengo ya Kituo cha Afya Kwihancha

Taarifa iliyosomwa kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa inaonesha kuwa mradi huo ambao upo hatua za mwisho unatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 mwezi ujao. 

“Mheshimiwa Mwenyeki wa CCM Wilaya ya Tarime, mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kwihancha unatarajiwa kukamilika tarehe 30/10/2023 kwa majengo yote,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ambayo ilisomwa na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Gibaso, Vitus Nyoni. 

Nyoni alitaja majengo ya kituo hicho cha afya na asilimia ya kazi ya ujenzi iliyofikiwa ikiwa kwenye mabano kuwa ni OPD (95 %), maabara (95%), jengo la mama na mtoto (85%), jengo la upasuaji (85%) na jengo la kufulia ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 50. 

Habari njema ni kwamba tayari kiasi chote cha shilingi milioni 600 kilishaidhinishwa na kutumwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na kazi inaendelea kwa kasi. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime, Solomon Shati, maandalizi ya kufungua kituo hicho yanaendelea na tayari kimeshaombewa fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba ili kianze kuhudumia wananchi. 

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Shaib Kaim alikagua na kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho na alieleza pia kufurahishwa na mradi huo, akisema umezingatia viwango vya ubora na kuaksi thamani ya fedha (value for money). 

Kaim alisema kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi. 

“Naipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari Mama Shupavu, Dktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya, na wana-Tarime tumeona, mwenye macho haambiwi tazama, ni historia, hakika Rais anaupiga mwingi sana,” alisema Kaim. 

Idadi ya miradi ya maendeleo iliyotembelewa na Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni saba, yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3.

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages