NEWS

Monday 30 October 2023

VTC YA PROFESSOR MWERA FOUNDATION, Kisima cha kuchota ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa



Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera, Hezbon Peter Mwera akifafanua jambo mbele ya baadhi ya majengo ya Tarime Vocational Training College.
-------------------------------------------

NA GODFREY MARWA
----------------------------------
 

WANACHUO zaidi ya 150 wa Tarime Vocational Training College (TVCT) kinachomilikiwa na Professor Mwera Foundation (PMF), wiki iliyopita waliwasilisha taarifa za mafunzo kwa vitendo waliyopata katika taasisi na mikoa mbalimbali nchini. 

Hafla hiyo ilifanyika chuoni hapo, ikihusisha makundi 27 ya wanafunzi waliosoma fani 11 tofauti zikiwemo za ufundi magari, umeme, uchomeleaji, udereva, kompyuta, ukatibu muhtasi, ushonaji, usimamizi wa hoteli na utalii, usaidizi katika maabara na uendeshaji biashara. 

Katika mawasilisho ya taarifa zao, wanachuo hao walisema mafunzo yao yalikwenda vizuri licha ya kukutana na changamoto ndogondogo. 

Hata hivyo, walishauri uongozi wa chuo hicho kujiimarisha katika vifaa vya kujifunzia kwa manufaa ya wanachuo kwa ujumla. 

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera ambaye aliwapongeza wanafunzi hao na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo waliyotoa kuhusu nini kifanyike ili kuboresha zaidi mazingira ya mafunzo kwa vitendo. 


Wanachuo ukumbini

Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa alitumia nafasi hiyo kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa za elimu ya ufundi zilizopo katika chuo hicho. 

“Wananchi wa Tarime na mkoa wa Mara changamkieni fursa ya elimu iliyopo hapa, karo zetu ni rafiki sana, waleteni vijana wote hata wa kike walioshindwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua wapate elimu ya ufundi ili waweze kufikia ndoto zao,” alisema. 

Hezbon pia alitoa wito kwa vyuo vya ufundi kuwa na utaratibu wa kuwapa wanafunzi nafasi ya kuwasilisha waliyojifunza kwa vitendo wanaporejea vyuoni. 

“Wakuu wa vyuo vya ufundi waweke utaratibu wa wanafunzi kuwasilisha taarifa ya mafunzo wanaporejea kutoka ‘field’ ili tuweze kufahamu changamoto zilizopo na kuzitafutia suluhisho,” alisisitiza. 

Mkurugenzi huyo alisema taasisi yake imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana ili kuwaandaa kuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. 

Aliongeza kuwa wamejikita zaidi katika kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi wakati wanasubiri matokeo ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na sita, na hata darasa la saba ili kupata stadi za ufundi zitakazowawezesha kujiajiri, au kuajiriwa na hivyo kuondokana na utegemezi katika familia na jamii kwa ujumla. 

Mbali na Tarime Vocational Training College, Taasisi ya Professor Mwera pia inamiliki Shule ya Sekondari Tarime Mchnganyiko na vyombo vya muziki kwa ajili ya kujenga na kukuza vipaji kwa wanachuo. 

Hivi karibuni, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliipatia Taasisi ya Professor Mwera kibali cha kufanya kazi zake na mikoa yote nchini baada ya kufanya vizuri katika mikoa 10 ya awali. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages