NEWS

Monday 30 October 2023

Waziri Bashe: Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji Bugwema utakuwa wa kwanza kwa ukubwa Kanda ya Ziwa



Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

NA MWANDISHI WETU
----------------------------------- 

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mradi wa umwagiliaji Bugwem uliopo Musoma Vijijini, Mara utakuwa wa kwanza kwa ukubwa katika Kanda ya Ziwa Victoria. 

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano na mkandarasi atakayeutekeleza juzi, Waziri Bashe alisema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendeleza mradi huo uliobuniwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. 

“Tunaamini kwamba ndani ya kipindi cha miezi sita tutaanza shughuli [utekelezaji], na nimemwambia mkandarasi na Tume ya Umwagiliaji kwamba huu mradi lazima uanze kutekelezwa, hakuna sababu ya kuchelewa,” alisema huku akidokeza kuwa hayo ni maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. 

“Hii kwetu ni hatua muhimu sana, ni mradi ambao nchi yetu imeusubiri kwa muda mrefu - toka wakati wa Rais wa Awamu ya Kwanza,” Waziri Bashe aliongeza na kubainisha kuw mradi huo una eneo lenye ukubwa wa hekta 30,000 lakini kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wataanza na hekta 10,000. 

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo ambaye amekuwa ‘akipigania’ uendelezaji wa mradi huo ameipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuidhinisha bajeti ya kuutekeleza. 

Kwa mujibu wa Prof Muhongo, tayari kazi ya upembuzi yakinifu ya mradi huo imeanza. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages