NEWS

Friday, 20 October 2023

Wanawake waombwa kukemea uvamizi mgodi wa Barrick North Mara



Afisa Mahusiano Msaidizi wa Mgodi wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu (mwenye suruali ya bluu) akipokewa kwa shangwe kuingia kwenye Mahafali ya 13 ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Ingwe wilayani Tarime, jana Oktoba 19, 2023.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
-------------------------------------------


WANAWAKE wameombwa kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya uvamizi vinavyofanywa na baadhi ya watu kwenye Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania. 

“Akina mama sisi ndio jamii yenyewe, sisi ndio washawishi, sisi ndio tunaojenga familia, hivyo tunapaswa kuwaongoza vijana wetu, watoto wetu, wababa na watu wote kuishi kwa kufuata sheria na kuondokana na vitendo vya kuvamia mgodi,” amesema Afisa Mahusiano Msaidizi wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu. 

Nasieku aliyasema hayo jana Oktoba 19, 2023 katika Mahafali ya 13 ya Wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo kilomita chache kutoka mgodini hapo. Nasieku ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo kwa niaba ya Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi. 

Aliwahimiza wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne shuleni hapo kujiandaa vizuri kwa ajili ya mitihani yao ya kitaifa, ili waweze kusonga mbele kimasomo na baadaye kuwa viongozi na watendaji bora katika ujenzi wa Taifa. 

“Tunaendelea kuwaombea na msimamie vitu vitatu; nidhamu, bidii na sala ili muweze kufanya mitihani yenu vizuri na kupata matokeo mazuri,” alisema Nasieku. 

Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ingwe, Mwalimu Joyce pamoja na mambo mengine alisema shule hiyo ina wanafunzi 1,390 (wasichana 785 na wavulana 605) wa kidato cha kwanza hadi cha sita, na kwamba wanaohitumu kidato cha nne ni 192 wakiwemo wavulana 100 na wasichana 92. 

Kwa mujibu wa risala hiyo, huduma ya maji ya uhakika ni mojawapo ya changamoto zinazoikabili shule hiyo. 

Shule ya Sekondari Ingwe ipo kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages