NEWS

Monday 23 October 2023

Ushirika wa WAMACU unavyoleta mageuzi ya kilimo Mara



Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye akiwa amesimama kwenye moja ya mashamba ya mahindi yaliyostawi kutokana na mbolea ya ruzuku.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu 
---------------------------------

NI mwendo wa kutaka kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo mkoani Mara. Ndivyo tunavyoweza kuelezea mipango ya kimkakati inayoendelea kushika kasi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd). 

Wiki iliyopita, chama hicho kilitwaa Tuzo ya Chama Bora cha Ushirika katika Usambazaji wa Mbolea ya Ruzuku Kanda ya Ziwa. 

Tuzo hiyo ilitoletwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani Tabora, Oktoba 13, 2023. 

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye, chama hicho cha ushirika kimefanikiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea iliyokuwa inawakabili wakulima wa mkoa wa Mara kwa miaka mingi. 

“WAMACU tumetatua changamoto ya mbolea kwa wakulima na sasa tunawafikishia wakulima mbolea ya ruzuku kwa wakati,” Gisiboye alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili mara baada ya WAMACU kushinda tuzo hiyo ya kufanya vizuri katika usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima. 

Wakulima wa mkoa huo sasa wanaiona WAMACU kama mkombozi wao, wakionesha matumanini ya kuongeza uzalishaji wa mazao ili waweze kujikamua kiuchumi. 

“Kwanza wakulima tulikuwa tunapata shida - sio tu kupata mbolea kwa wakati, bei ilikuwa kubwa lakini sasa WAMACU wanatupatia mbolea ya ruzuku kwa bei ya shilingi 70,000 kwa mfuko wenye kilo 50, badala ya shilingi 150,000 kabla ya WAMACU,” anasema Elias Samwel, mkulima na mwakilishi wa wakulima kutoka AMCOS ya kijiji cha Kangariani wilayani Tarime. 

Elias anasema mbolea hiyo inawasaidia kupanda mazao mbalimbali kama vile mahindi, kahwa na viazi ulaya katika kijiji chao kama ilivyo kwenye vijiji vingi wilaya humo. 

Pamoja na mambo mngine, wilaya ya Tarime inaongoza katika kuzalisha kahawa aina ya Arabica ambayo inatamba kwenye soko la dunia kutokana na mwonjo wake wa kipekee, kwa mujibu wa wataalmu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI). 

“Kipindi cha nyuma kabla ya WAMACU tulikuwa tunategemea mbolea kutoka nchi jirani ya Kenya, lakini sasa hivi tatizo hilo limebaki historia,” anaongeza mkulima huyo. 

WAMACU Ltd ilianza kusamba mbolea ya ruzuku kwa wakulima Novemba 2022. 

GM Gisiboye anataja aina za mbolea za ruzuku ambazo WAMACU inauza kwa wakulima kwa sasa kuwa ni DAP, ULEA, NPSzn na NPS-B. 

Katika msimu huu pekee ambao ulianza Mei mwaka huu, chama hicho kimeuza mbolea ya ruzuku takriban tani 1,723 kwa wakumilma wa mkoani Mara. 

“Tuna vituo kila halmashauri ya mkoa huu ili kuhakikisha huduma hii inawafikia wakulima kwa wakati,” anafafanua GM Gisiboye. 

Anasema uhitaji wa mbolea ya ruzuku unazidi kuongezeka kila siku - jambo ambalo linaonesha tija kwa kwa wakulima. 

“Kadiri ya uhitaji wa mbolea unavyoongezeka na uzalishaji unaongezeka. Hivyo kuna kilimo cha tija, tunataka kuendeleza hii tija ili wakulima wengi wanufaike zaidi,” anaongeza. 

Anasema WAMACU imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika kusaidia wakulima kuwa na uzalishaji wenye tija na hivyo kuwezesha nchi kuwa na chakula cha kutosha (food security). 

“Mpango wetu kama WAMACU Ltd ni kuhakikisha mbolea ya ruzuku sio tatizo tena katika kuwafikia wakulima,” GM Gisiboye anasisitiza. 

Mipango ya WAMACU 
Meneja Mkuu Gisiboye anasema WAMACU ina mpango wa kuanza kusaidia wakulima kutafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya mazao mbalimbali wanayozalisha. 

Mbali na kahawa, mazao mengine yanayostawi katika mkoa wa Mara ni mahindi, viazi, ndizi, mtama, muhogo, nyanya, vitunguu, alizeti na pamba. 

“Tumejipanga vizuri kuanza kutafuta masoko yenye bei nzuri ya mazao ya wakulima wetu na pia kuyaongea thamani mazao yao,” alidokeza Gisiboye. 

WAMACU Ltd ni miongoni mwa Vyama Vikuu vya Ushirika vilivyopewa dhamana ya kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima, kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP. 

Chama hicho kinajishughulisha na ukusanyaji wa kahawa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuiongezea thamani na kuitafutia masoko ya nje. 

Lakini pia kwa sasa WAMACU ina leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea ya ruzuku kutoka TFRA. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages