--------------------------------------------
Mara Online News
-------------------------
SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) limefanya ukaguzi shirikishi wa miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, misitu na mazingira iliyotekelezwa mkoani Mara.
Katika ziara hiyo, Shirika la WWF limeshirikiana na wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria - Dakio la Mara kufanya ufuatiliaji wa miradi hiyo.
Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Mafunzo kutoka WWF, Enock Edward Rutaihwa alishirikiana na wataalamu kutoka Dakio la Mara, Joseph Masaka (Msimamizi wa Kitengo cha Mazingira) na Norbeth Zeno Honde (Mtaalamu wa Maji) katika ziara hiyo.
Wametumia muda wa wiki mbili katika ziara hiyo iliyomalizika wiki iliyopita, kwa lengo la kujionea na kufanya tathmini ya maendeleo ya miradi hiyo na manufaa yake kwa jamii. Miradi waliyokagua ni ambayo imepata misaada mbalimbali kutoka Shirika la WWF.
Ukaguzi wa miradi ukiendelea
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na wataalamu hao ni pamoja na uhifadhi wa chanzo cha kisima cha maji Kibeyo katika kata ya Kisangura wilayani Serengeti, uliofadhiliwa na WWF.
Wakiwa katani Kisangura, walifuatana na Mshauri na Mlezi wa Jumuia za Watumia Maji Bonde la Mto Mara, Lameck Nyasagati, ambapo pia walihimiza wakulima kulima kitaalamu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Pia katika kata ya Rung’abure wilayani humo, walitembelea mradi wa ufugaji nyuki kwa lengo la kutunza misitu, unaoendelea kufanya vizuri.
Mfugaji wa nyuki, Willison Chorwa alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali, mashirika na wadau wengine kumsaidia kupata soko la uhakika la asali anayovuna katika mradi huo.
“Soko ni changamoto kwangu, nina mizinga 80, hata sasa nina lita 70 za asali mbichi ndani kwenye madumu, sina pa kuiuza, nauza rejareja kwa shida. Naomba serikali yetu, mashirika na wadau wanisaidie kupata soko,” alisema Chorwa na kubainisha kuwa huvuna lita 200 za asali kwa msimu (miezi sita).
Mfugaji wa nyuki, William Chorwa (katikati) na wataalamu wa mazingira wakionesha sehemu ya asali aliyovuna wilayani Serengeti.
Walitembelea pia kisima cha maji Miseke katika kata ya Manchira wilayani Serengeti, ambapo walipokewa na Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Miseke, Kennedy Osodo.
Osodo ambaye pia Mjumbe wa Kamati ya Bwawa la Maji Manchira, alisema kisima hicho hakikauki maji na kwamba ni tegemeo pekee la wanakijiji.
Wataalamu wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira wilayani Serengeti
“Kisima hiki kilichimbwa na wazee wetu mwaka 1970, hakijawahi kuisha maji hata jua liwake mwaka mzima. Tunawashukuru wafadhili wetu WWF wanakuja mara kwa mara kutuelimisha namna bora ya kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda miti na kutoingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji,” alisema.
Kwenye mradi wa miti Somoche wilayani Serengeti, walikuta miti 580 kati ya 620 iliyotolewa na WWF imekua vizuri katika eneo lenye ukubwa wa ekari nane. Walikagua pia tenki la maji lililotolewa msaada na shirika hilo katika Shule ya Sekondari Somoche.
Makutano ya mto Mara na mto Tobora
Waliridhishwa na ukuaji wa miti kando kando ya makutano mto Mara na mto Tobora katika kijiji cha Merenga kilichopo kata ya Nyansurura, Serengeti, ambapo WWF iliwezesha miti 2,068 kwenye kikundi cha uhifadhi wa mazingira kinachofanya kazi chini ya Jumuia ya Watumia Maji Tobora Chini.
Lazaro Chacha, mwanakikundi cha uhifadhi wa mazingira makutano ya maji ya mto Tobora na mto Mara, alisema “Sisi tunasaidiana na serikali kutunza mito hii na mazingira yake.”
Kisha walifika na kukagua maendeleo ya kisima cha Mwanahaba katika kijiji cha Nyamatoke, kata ya Mosongo, Serengeti, ambacho kilikarabatiwa mwaka 2009 kwa ufadhili wa WWF.
Mwonekano wa sehemu ya kisima cha Mwanahaba
Mmoja wa wanufaika wa kisima hicho, Bhoke Mwita, aliwashukuru WWF na kuiomba serikali kuwaunganishia maji ya bomba majumbani kutoka kwenye chanzo cha Mwanahaba chenye maji ya uhakika.
“Tunawashukuru sana WWF kwa kukarabati kisima chetu, hatujawahi kuwa na uhaba wa maji kwenye kisima cha Mwanahaba. Shida yetu tunachangia maji na wanyama, tunaomba serikali na WWF ituunganishie maji kwa mabomba kutoka Mwanahaba,” alisema Bhoke.
Wataalamu wakikagua shamba la mkulima Chacha Mugini (nyuma)
Wakiwa wilayani Tarime walitembelea shamba la mkulima Chacha Mugini katika kijiji cha Tagare, kata ya Mriba, mmoja wa wakulima waliokwisha kupata mafunzo maalumu ya kilimo cha kutumia mbinu ya makinga maji kwenye maeneo yenye mtelemko mkali.
Walifurahia kukuta mkulima huyo akiendelea kutekeleza kwa vitendo yale waliyofundishwa chini ya ufadhili wa WWF.
Mtoto akichota maji katika kisima cha Nyaitembe
Kwingineko katika kijiji cha Kangariani kilichopo kata ya Itiryo wilayani Tarime, wataalamu hao waliahidi kutoa msaada wa kukijengea kisima cha maji Nyaitembe miundombinu maalumu. Pia walikagua vigingi vilivyowekwa na WWF ili kuzui shughuli za kibinadamu kufanyika ndani ya mita 60 ya eneo la kisima hicho.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kangariani, Suleman Gisiri aliwashukuru WWF kwa kuendelea kufadhili shughuli za uhifadhi kisima hicho kinachohudumia wananchi zaidi ya 500.
Katika ziara hiyo, walikutana pia na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Matongo wilayani Tarime, Daniel Amos Kikerero, Mshindi wa Tuzo kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki aliyeibuka Mchoraji Bora wa Bonde la Mto Mara, akionesha athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu katika bonde hilo.
Wataalamu hao walifika shuleni hapo kufuatilia maendeleo ya mradi wa upandaji miti 1,000 iliyotolewa na WWF mwaka 2021. Kisha walielekea kijiji jirani cha Nyabichune kukagua maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa kupima afya ya maji ya mto Tighite.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Matongo wakipima afya ya mto Tighite
Pia walieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi wa shamba la Baraki Sisters unaoendeshwa chini ya Kanisa Katoliki wilayani Rorya.
Baraki Sisters ni miongoni mwa wakulima waliopata mafunzo ya mbinu bora za kilimo katika chuo cha Mogabiri kilichopo Tarime, chini ya ufadhili wa WWF. Mafunzo hayo yalihusu kilimo kinachohifadhi mazingira na kutoa mavuno mengi katika eneo dogo.
Wataalamu wakiongozwa kukagua mradi wa shamba wa Baraki Sisters wilayani Rorya
Sista Cecilia Kasanda wa Baraki Sisters Farm alisema mafunzo waliyopata ya uandaaji mashamba na mbolea kitaalamu yamekuwa na manufaa makubwa kwao.
“Zamani tulipata magunia saba hadi 10 kwa ekari moja, lakini baada ya mafunzo tumegundua kuwa tunaweza kupata magunia 20 na kuendelea kwa ekari moja. Tunawashukuru WWF kwa hiki walichotufundisha, tunaomba waendelee kusaidia Watanzania wasiokuwa na elimu hii ya kilimo,” alisema Sista Kasanda.
Mabwawa ya ufugaji wa samaki kijijini Utegi, Rorya.
Walifika pia kwa Mericiana Thomas Rhobi, mfugaji wa samaki kwenye mabwawa matatu katika kijiji cha utegi, kata ya Koryo wilayani Rorya, ambapo waliridhishwa na maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 6.3.
Wakiwa wilayani Butiama, wataalamu hao walikagua tenki la maji lenye ujazo wa lita 1,000 na miti vilivyotolewa msaada katika Shule ya Msingi Kwisaro.
Kikundi cha uoteshaji miti kijijini Kwisaro, Butiama.
Walikuta kati ya miti 750 waliyopeleka, iliyokua ni 250. Mingine 500 haikuota kutokana na udongo wa chumvi chumvi na kuharibiwa na mifugo ya wanakijiji.
Tenki la maji ambalo Shirika la WWF lilitoa msaada katika Shule ya Msingi Kwisaro
Hata hivyo, shule hiyo iliomba WWF iwaongeze msaada wa miti 500 inayoweza kuhimili udongo wenye chumvi chumvi nyingi na kuvuta maji kutoka kwenye tenki la RUWASA lililopo umbali wa kilomita moja kutoka shuleni hapo.
Wadau wa mazingira katika picha ya pamoja wilayani Tarime
Kwa ujumla, wasimamizi wa miradi na wanavijiji husika walilishukuru Shirika la WWF kwa kuwapiga jeki katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, misitu na mazingira.
Juhudi za WWF zimesaidia kurejesha hifadhi ya msitu iliyokuwa hatarini kutoweka na wanafunzi wa shule mbalimbali wamepatiwa elimu ya awali na vitendea kazi vya kupima afya ya mito kupitia wadudu wanaoishi majini.
Lakini pia shirika hilo limewezesha jumuiya ya watumia maji katika Bonde la Mto Mara kuanzisha miradi ya uoteshaji miche ya miti kwa ajili ya kujipatia kipato na kuhifadhi mazingira.
Kwa mujibu wa Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Mafunzo, Enock Edward Rutaihwa, jukumu kubwa la WWF ni kuwapa wananchi elimu ya uhifadhi na utunzaji vyanzo vya maji na mazingira hai katika dakio la Mto Mara.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment