NEWS

Monday 6 November 2023

DC Mntenjele akagua ujenzi wa VETA Nyamongo, atoa maelekezoMkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (kulia mbele) akisikiliza maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa VETA Nyamongo, Ramadhani Magimba (mwenye faili), jana Jumatatu.
------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Nyamongo
Mara Online News
-----------------------------


MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Kanali Michael Mntelenje, jana Jumatatu alikagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) Nyamongo, na kutaka utekelezaji wa mradi huo uharakishwe.

“Kazi inaenda vizuri, ingawa kuna changamoto ya mvua inayoendelea kunyesha, huyo ‘supplier’ anayeleta molamu ajitahidi kutafuta vyanzo vingine kama kule anakochukua molamu kuna changamoto ya kukwama. Kazi ikikwama malengo ya kukamilika kwa chuo hiki mwakani [2024] hayatafikiwa,” DC Mntenjele alisema.

Aliongeza: “Tunataka chuo hiki kikamilike vijana wajifunze hapa ufundi ili wapate njia mbadala ya kuendesha maisha yao, badala ya kutegemea kuingia mgodini kugombana na walinzi na kusababisha changamoto za uzalishaji kwenye mgodi.”

Ujenzi wa VETA Nyamongo ukiendelea
Awali, Msimamizi wa mradi huo, Ramadhani Magimba, alimweleza DC Mntenjele kwamba mvua zinazonyesha na kutojitokeza kwa vibarua vinachangia kuchelewesha ujenzi wa chuo hicho.

“Mradi umefikia asilimia 20, na awamu ya kwanza utagharimu bilioni moja na milioni mia nne. Ujenzi upo ngazi ya msingi, tulitarajia kufikia kwenye finishing [ukamilishaji] mwezi wa nne kama kusengekuwa na changamoto ya mvua. Pia tunaomba vijana waje kufanya kazi - chuo kipo kwao - waje kufanya kazi na kujifunza elimu kwa vitendo kutoka kwa mafundi,” alisema Magimba.

Pamoja na mambo mengine, ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kusaidia kupunguza vitendo vya kuvamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi wa ujenzi wa VETA Nyamongo, DC Mntenjele alifuatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Solomon Shati.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages