NEWS

Saturday 11 November 2023

Magonjwa yasiyoambukiza yaipeleka Hospitali ya Bugando Nyamongo
Na Joseph Maunya, Nyamongo
Mara Online News
-----------------------------


HOSPITALI ya Rufaa Bugando (BMC) iliyopo jijini Mwanza, imeshiriki maonesho ya wajasiriamali yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyamongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, kwa ajili ya kutambua magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, matatizo ya usikivu na kutoa ushauri tiba kwa watu mbalimbali.

Daktari bingwa wa magonjwa ya tiba, Dkt Raymond Wilson kutoka kliniki ya madaktari bingwa ya MBC, alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika maonesho hayo yaliyopewa jina la 'Twende Mara Nyamongo - Expo 2023'.

Dkt Raymond Wilson
“Lengo hasa ni kutambua magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yamekuwa tatizo kubwa kwa sasa hivi. Watu wengi wana shida lakini hawajitambui, hivyo tunahitaji kuwafikia watu wengi na kuwapa elimu ya kujikinga na mpaka leo tumepima watu 507, kati ya hao, 215 wana uzito uliopitiliza, 102 wana shinikizo kubwa la damu, 20 wana kisukari na 20 wana tatizo la usikivu, na wote tumewapa ushauri, tiba na rufaa kwa matibabu zaidi,” alisema Dkt Raymond.


“Nawashauri wananchi wenzangu wafike ili wapime afya zao na wapate ushauri, lakini pia Serikali iangalia namna ya kuwezesha hawa wataalamu wawe wanakuja mara kwa mara kutusogezea huduma kama hizi,” alisema Sinda Mwita Kichere, mkazi wa kijiji cha Nyangoto baada ya kupata huduma katika banda la BMC.


Kwa upande wake Hamisi Masasa ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Powerlife Organic Wellness Tanzania Ltd inayojihusisha na tibalishe, alisema wameandaa na kudhamini maonesho hayo ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo kukuza biashara zao, lakini pia kuwaunganisha na taasisi za kifedha ziwasaidie kukuza mitaji yao.

CEO Hamisi Masasa
Kwa mujibu wa Masasa, tayari kampuni hiyo imeendesha maonesho ya aina hiyo katika miji ya Musoma na Sirari, kwa lengo la kuuwezesha mkoa wa Mara kuwa miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza katika uchangiaji wa pato la taifa.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages