NEWS

Sunday 12 November 2023

Serengeti Safari Marathon 2023 yaingia dosari, washiriki wakiwemo watoto wasononeka
NA MWANDISHI WETU, Serengeti
Mara Online News
-------------------------

MBIO maarufu za Serengeti Safari Marathon (SSM) zimeingia dosari mwaka huu, baada ya washiriki kulalamika kutopewa medali na huduma nyingine muhimu kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka iliyopita.

Viongozi wa vilabu vya mazoezi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo ya Kanda ya Ziwa wameeleza kusikitishwa na hali hiyo, wakisema inaweza kuua mbio hizo ambazo zilikuwa zinasaidia kutangaza utalii wa ndani na nje katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kama ilivyo ada, mbio hizo jana Jumamosi zilifanyika kuanzia lango la Ndabaka lilipo katika hifadhi hiyo, juzi Jumamosi.

Mwenyekti wa Klabu ya Tarime Runners, Lusako Maurice, ametaja kasoro kubwa walizokumbana nazo kuwa ni kukosekana kwa medali na viburidisho kama vile chai na juice kwa washirki kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka ya nyuma.

“Ikumbukwe kuwa watu wengi wamekuwa wakishiriki kwa lengo la kupata medali kama kumbukumbu na kufurahia kukimbia ndani ya hifadhi yetu ya Serengeti,” Lusako ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo Jumapili, akisisitiza kuwa hali hiyo imewahuzunisha na kuwakatisha tamaa.

“Hizi changamoto zimesababisha sisi viongozi wa klabu kuonekana kama matapeli, ukizingatia baadhi ya wanachama ni wapya na walitaka kuona kwa macho yao yale mazuri tuliyokuwa tunayasimulia kuhusu Serengeti Safari Marathon,” amesema Lusako.

Ameongeza: “Hali hii itasababisha tusiaminike tena pale inapotokea tunashawishi wanachama wetu kuhudhuria mbio nyingine.”Washiriki wengi wamelaani hali iliyojitokeza katika mbio hizo za mwaka huu, wakisema haifai kutokea katika hifadhi bora kama Serengeti.

“Watu tumetumia fedha na kuamka usiku wa manane lakini hakuna kilichokuwa kinaeleweka,” amesema mmoja wa washiriki hao.

Wengine wameapa kutoshiriki tena katika mbio hizo kutokana na dosari kubwa zilizojitokeza.

“Kwa kweli Serengeti Safari Marathon mwaka huu ‘zimefeli’. Mfano mimi nimeenda na watoto wangu washirki ili wapate medali lakini hakuna medali, kama hiyo haitoshi unamaliza mbio hakuna hata sehemu ya kunywa juice au maji,” amesema Chacha Mwihechi(MC) kutoka jijini Mwanza.

Mbio hizo zilipata umarufu mkubwa katika miaka miwili iliyopita huku washiriki wakitoka ndani na nje ya nchi.

Viongozi wa vilabu vya wakimbiaji walioshiriki mbio hizo za mwaka huu wamelazimika kuwaomba radhi wananchama wao huku wakituhumu waandaji.

“Bila medali ni kazi bure,” mmoja wa wakimbiaji na wapenzi wa mbio hizo ameandika kwenye mitandao ya kijamii.

Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kuwa mgeni rasmi wa Serengeti Safari Marathon mwaka 2020 katika eneo hilo hilo la Ndabaka na kutaka mbio hizo kuendelezwa ili zitumike kutangaza na kuvutia watalii wengi wanaotembelea hifadhi ya Taifa Serengeti.

Waandaji wa Serengeti Safari Marathon 2023 kupitia taarifa yao kwa umma ambayo Sauti ya Mara imeiona, wameomba radhi washiriki wa mbio hizo wakisema medali zilichelewa kutoka nchini China.

“Tunaomba radhi na kuwafahamisha washiriki, mashabiki, wadhamini, washirika na wapenzi wa Serengeti Safari Marathon kwamba hatujapokea medali hadi sasa kwa ajili ya mbio zilizofanyika tarehe 11, 2023,” imesema ya taarifa hiyo iliyosainia na Henry Kimambo, Mkurugenzi.

Hata hivyo, walisema wanafanya jitihada za kuhakikisha kuwa kila mshiriki wa mbio hizo anatumiwa mara zitakapowasili na kwamba watazigawa kupitia vituo vya Arusha, Bunda, Dar es Salaam, Dodoma, Geita na kwa viongozi wa vikundi au vilabu vilivyowaandikisha ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa taarifa yao hiyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages