Paul Makonda
Mara Online News
--------------------------
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, amewasilisha kwa uongozi wa chama hicho tawala ngazi ya Taifa ombi la kuipandisha hadhi wilaya hiyo kuwa mkoa.
Ngicho amewasilisha ombi hilo kwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda katika mkutano wa hadhara mjini Tarime leo Novemba 14, 2023.
Baadaye katika hotuba yake, Makonda amesema amepokea ombi hilo na kuahidi kulifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati huo huo, Makonda amemwagiza Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda, kuingilia kati ili pikipiki (bodaboda) zilizokamatwa na Jeshi la Polisi katika mji wa Sirari mpakani na nchi ya Kenya, ziachiwe na kukabidhiwa kwa wamiliki husika, na katika mazingira yaliyo rafiki kufikia kesho Jumatano.
"Kuanzia sasa Mhe. Mtanda ifikapo kesho pikipiki zote zilizokamatwa Sirari warudishiwe wenye pikipiki zao, na kama kuna mali zilizokamatwa watozwe kodi wapewe mali zao, na kuanzia hapo utaratibu wa kisheria ufuate mkondo wake," amesema Makonda.
Sambamba na hilo, Katibu huyo wa NEC ya CCM Taifa amemwagiza RC Mtanda kushughulikia haraka utatuzi wa migogoro ya ardhi inayodaiwa kukithiri katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment