NEWS

Friday 3 November 2023

Serikali yatangaza mabadiliko Sera ya Elimu na Mafunzo, elimu ya msingi sasa kukomea darasa la 6Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza Bungeni
--------------------------------------

NA MWANDISHI
WETU, Dodoma
-------------------------


SERIKALI imefanya mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo, ambapo pamoja na mambo mengine, elimu ya msingi nchini sasa itakomea darasa la sita, badala ya darasa la saba. 

Mabadiliko hayo yalitangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni Dodoma jana Alhamisi, akifafanua kuwa pendekezo hilo litaanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2027. 

Aidha, Wazirili Mkuu alisema elimu ya lazima sasa itakuwa ya miaka 10 badala ya miaka saba. “Elimu hiyo ya lazima itajumuisha elimu ya msingi ya miaka sita na elimu ya sekondari ya chini ambayo itatolewa kwa miaka minne,” alifafanua. 

Alisema utekelezaji wa pendekezo hilo utafanyika sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba, na badala yake kuanza kufanyika kwa tathmini ya darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari. 

Majaliwa alitaja mabadiliko ya pili kuwa ni kuongeza fursa za elimu ya amali kwa maandalizi ya elimu ya ufundi na mafunzo stadi, ambayo itakuwa ikitolewa kuanzia kidato cha kwanza. 

Mabadiliko ya tatu, alisema ni elimu ya ualimu kuanza kutolewa kwa wahitimu wa kidato cha sita na kuendelea. 

Alitaja mabadiliko ya nne ya Sera ya Elimu na Mafunzo kuwa ni mafunzo ya ualimu kujumuisha mwaka mmoja wa mafunzo chini ya uangalizi baada ya kuhitimu mafunzo tarajari. 

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tano ni kwenye upimaji, ambapo Serikali itauhuisha mfumo wa upimaji na tathmini kwa kuzingatia umahiri hitajika kwa kila ngazi, kwa lengo la kuwa na upimaji endelevu na matumizi ya mbinu mbalimbali za upimaji na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi katika kujifunza. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages