NEWS

Sunday 19 November 2023

TaCRI yahimiza wakulima Kanda ya Ziwa kuchangamkia miche bora ya kahawa kwenye vitalu vyake



Meneja wa Kanda wa TaCRI - kituo kidogo cha Sirari, Almas Hamad akifafanua jambo wakati wa Maonesho ya Nane ya Kilimo Mseto mjini Musoma, ambayo yalihitimishwa juzi.
-----------------------------------------------

NA MWANDISHI
WETU, Musoma
--------------------------


TAASISI ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) imetoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa ya miche bora ya kahawa katika vitalu vyake vilivyopo maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Tunawaomba wakulima waje wapate elimu na tutawapatia miche bora bure,” Meneja wa Kanda wa TaCRI - kituo kidogo cha Sirari, Almas Hamad amesema.

Hamad aliyasema hayo wakati wa Maonesho ya Nane ya Kilimo Mseto – ambayo yalihitimishwa mjini Musoma juzi. Banda la TaCRI lilivutia mamia ya wananchi waliotembelea maonesho hayo.

Hamad alisema TaCRI ina vitalu vikubwa vya kuzalisha miche bora ya kahawa katika wilaya za Tarime, Serengeti, Butiama, Ukerewe na Buchosa.

Kitalu cha miche bora ya kahawa
Alisema TaCRI imejizatiti kutoa elimu kwa wakulima kwa kushirikiana na maofisa ugani ngazi ya kata na kijiji.

Kwa mujibu wa meneja huyo, lengo la TaCRI ni kuendelea kufanya tafiti ambazo zitasaidia kuinua wakulima wa kahawa.

“Lengo letu ni kufanya tafiti zinazoleta matokeo chanya kwa mkulima. Changamoto ni rasilimali pesa, tafiti zinahitaji pesa nyingi,” alisema Hamad, huku akiomba Serikali kuiongezea taasisi hiyo fedha kwa ajili ya kufanikisha malengo yake ya kuendeleza sekta ya kahawa.

TaCRI ni miongoni mwa wadau muhimu ambao wamesaidia kufufua kilimo cha kahawa aina ya Arabica katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Kahawa hiyo ya Tarime kwa sasa inatamba katika soko la dunia kwa ubora kutokana na kuwa na muonjo wa kipekee.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages