NEWS

Wednesday 20 December 2023

Jitihada za Mbunge Chege zawezesha vijana wa Rorya kupata mkopo wa pikipiki 253 kutoka Benki ya AzaniaMwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa (katikati) akimpongeza Mbunge wa Rorya, Jafari Chege (mwenye kofia anayecheka), kwa kuomba na kudhamini mkopo wa pikipiki 253 kutoka Benki ya Azania kwa ajili ya vijana jimboni humo jana Jumatano. (Picha na Godfrey Marwa)
-------------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Rorya
----------------------------------------


VIJANA 253 katika wilaya ya Rorya wamepata kila mmoja mkopo wa pikipiki mpya - wenye riba nafuu, ulioombwa na Mbunge Jafari Chege kutoka Benki ya Azania Tawi la Lamadi.

Vijana hao ambao ni maafisa wasafirishaji walikabidhiwa pikipiki hizo 253 na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa aliyekuwa katika ziara ya kikazi wilayani humo jana Jumatano.

Chandi alimpongeza Mbunge Chege kwa kuwajali vijana wa Rorya na kuwatafutia fursa hiyo ya kujikwamua kiuchumi - katika jitihada za kuisaidia Serikali kutengeneza ajira kwa kundi hilo la jamii.


Mwenyekiti Chandi (katikati) akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya pikipiki hizo.

“Kwa niaba ya CCM Mara ninakupongeza [Mbunge Chege] kwa kazi nzuri, umemsaidia Rais [Dkt Samia Suluhu Hassan] kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wetu, Mungu awasaidie.

“Endelea kukomboa vijana, pikipiki hizi zitawasaidia katika maisha yao, ninawasihi vijana zitumieni vizuri mpate faida, msaidie familia zenu,” alisema Chandi.

Awali, Mbunge Chege alisema aliomba na kujitolea kuwa mdhamini wa mkopo huo wa pikipiki kutoka Benki ya Azania, kwa sharti la kila mnufaika kurejesha shilingi 6,000 kwa siku.


Mbunge Chege (wa pili kushoto) akifurahia jambo wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo.

“Vijana wamekuwa wakipewa mikopo kwa riba kubwa ya kurudisha elfu kumi kwa siku, unajikuta unaendelea kuwa masikini, kwa kutambua hilo nikawatafutia pikipiki - marejesho yawe nusu ya kile mnacholipa,” alisema Mbunge huyo wa Rorya na kuahidi kuwaombea vijana wengine mkopo wa pikipiki 300.

“Tumezitoa hizi pikipiki bila kujali itikadi ya chama, tunataka kuunganisha Rorya, hatupaswi kubaguana kwa utarafa, ukoo na lugha, hata hizo mia tatu zinazokuja tutafanya hivyo kwa sababu tuna ‘focus’ kuunganisha wananchi wetu,” alisema Chege.

Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi wa wilayani Rorya kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia katika jitihada za kuleta maendeleo ya kisekta nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages