NEWS

Tuesday 26 December 2023

Matarajio yetu kwa Nyansaho katika Bodi ya Wakurugenzi TANESCODkt Rhimo Simeon Nyansaho
----------------------------------------

NA CHRISTOPHER GAMAINA
----------------------------------------


WIKI iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alimteua Mkurugenzi wa Mendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Dkt Rhimo Simeon Nyansaho kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).

Dkt Nyansaho anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo - ambaye aliteuliwa na Rais Samia kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

Tunampongeza Dkt Nyansaho kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais kuongoza Bodi hiyo. Kwa upande mwingine, Rais Samia naye anastahili pongezi kwa kumteua Dkt Nyansaho kushika nafasi hiyo.

Dkt Nyansaho ni msomi aliyebobea katika masuala ya biashara na uchumi. Ni mtu wa watu, chapakazi mahiri na mpenda maendeleo.

Rais ameonesha imani kubwa kwa Dkt Nyansaho, na anaamini hatamwangusha katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO.

Dkt Nyansaho ambaye ni mchumi kitasnia, amepewa dhamana ya kuongoza Bodi hiyo katika kipindi ambacho Watanzania wengi hawaridhiki na huduma ya umeme. Kipindi ambacho wananchi wanateseka kwa mgawo wa umeme. Kipindi ambacho umeme unakatika mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nchini, na mara nyingi bila wateja wa TANESCO kupewa taarifa.

Kwa kifupi, Dkt Nyansaho amepewa madaraka hayo kipindi ambacho watu hawaridhiki na upatikanaji wa huduma ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani na maeneo mengine ya biashara.

Kwa hiyo, Dkt Nyansaho atambue kuwa amepewa jukumu kubwa la kusimamia utendaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO na kutumia uwezo na uzoefu wake kusaidia utatuzi wa changamoto zinazokwaza usambazaji wa huduma ya umeme kwa kiwando cha kuridhisha.

Waswahili wanasema “hakuna mkate mgumu mbele ya chai”. Dkt Nyansaho ana uwezo na uzoefu mkubwa wa kusimamia kwa mafanikio taasisi za kibiashara ndani na nje ya nchi. Hivyo matumaini ya wengi ni kwamba anakwenda kusaidia kuleta mageuzi makubwa ndani ya TANESCO.

Rais Samia na Watanzania kwa ujumla watafurahi kuona na kusikia viongozi na watendaji wa TANESCO wanampokea vizuri Dkt Nyansaho na kumpatia ushirikiano wa dhati, ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi utakaoboresha huduma ya umeme nchini.

Tunajua Serikali yetu inaendelea na juhudi za kuimarisha na kuongeza mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, ikitambua kuwa huduma hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Kwa hiyo, tunaamini kwamba yajayo ndani ya TANESCO yenye Dkt Nyansaho yatawafurahisha Watanzania. Tunaamini kwa umahiri na uzoefu wake, ataishauri vizuri Serikali na wataalamu wake katika kuweka na kutekeleza mipango yenye tija kwa shirika hilo na wateja wake.

Hii ni sawa na kusema kwamba uenyekiti wa Dkt Nyansaho katika Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO hautakuwa na maana kama vilio vya wananchi dhidi ya huduma mbovu ya umeme vitaongezeka.

Hivyo basi, bila shaka Dkt Nyansaho amejipanga vizuri kuhakikisha uongozi wake katika Bodi hiyo unakidhi matarajio ya Rais Samia na Watanzania katika suala zima la kuboresha huduma ya umeme nchini.

Kikubwa, tumwombee Dkt Nyasaho baraka za Mwenyezi Mungu - amjalie uzima, afya njema na hekima katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kwa manufaa ya Taifa letu.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages