NEWS

Tuesday 26 December 2023

Nyambari azua mjadala mkubwa Tarime Vijijini



Nyambari Nyangwine
-------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU, Tarime
---------------------------------------------------


SIKU chache baada ya aliyewahi kuwa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine kutamka kwamba hataki ubunge, wananchi mbalimbali katika jimbo la Tarime Vijijini wametoa maoni - wakisema atakuwa hawatendei haki kwa uamuzi wake huo.

Nyambari ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd (NNGCL), alitoa kauli hiyo wakati alipokwenda kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga, Tarime Vijijini, ambapo shilingi zaidi ya milioni 200 zilipatikana.

Wakizungumza na Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti juzi na jana, wakazi mbalimbali wa Tarime Vijijini wakiwemo wanachama wa chama tawala - CCM, walisema Nyambari bado ni mtu muhimu kwao na hawawezi kusahau maendeleo makubwa aliyowaletea katika jimbo hilo.

“Nyangwine aliacha chapa (alama) kubwa ya maendeleo Tarime. Yeye ndiye alisaidia jimbo la Tarime likagawanywa kuwa mawili [Tarime Mjini na Tarime Vijijini]. Alifanya maendeleo makubwa ambayo hayajawahi kufikiwa mpaka sasa hivi.

“Hata ukienda Halmashauri ya Wilaya ya Tarime rekodi inaonesha kwamba miradi mingi ya maendeleo ya wananchi ililetwa na kutekelezwa wakati wa uongozi wa Nyambari Nyangwine kama mbunge, hakika alikuwa mbunge wa vitendo,” alisema mkazi wa kata ya Sirari, Marwa Mokare - maarufu kwa jina la Wainenga.

Wainenga aliongeza kuwa Nyambari ni mpenda maendeleo, ndio maana ameendelea kurudi Tarime na kushiriki kikamilifu katika harambee za kuchangia maendeleo ya wana-Tarime. “Hata michango midogo midogo anayotoa ni mingi, mkimwambia mna tatizo anaweka kitu,” alisema.

Alitaja alama nyingine ya maendeleo iliyowekwa na Nyambari kuwa ni msaada wa vyerehani kwa wajumbe wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika kata zote 32 za wilaya ya Tarime wakati huo - kabla haijagawanywa kuwa majimbo mawili ya uchaguzi, ambapo kila kata ilipata vyerehani vitatu.

Kwa mujibu wa Wainenga, Nyambari atakumbukwa pia kwa juhudi kubwa alizofanya kukomesha mapigano ya kikoo katika wilaya ya Tarime.

“Wakati wa uongozi wake alikataa mambo ya koo, alipoingia madarakani mapigano yalikata kabisa, alikusanya wazee wa mila kutoka koo zote za kabila la Wakurya akawapeleka Ikulu kwa Rais kuzungumzia masuala ya amani, na kutokea kipindi hicho amani ikatawala mpaka leo. Kwa hiyo sisi bado tunamhitaji sana, akija tutakimbia naye,” aliongeza.

Kwa upande wake, mkazi wa kata ya Nyamwaga, Ambrose Chacha aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga, alisema Nyambari ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza, mwadilifu na asiyependa chuki na ubinafsi.

“Huyu bwana wakati akiwa mbunge alikuwa kiongozi sahihi, ni mtu ambaye hana chuki moyoni mwake, na si mtu wa kujitukuza na kujiona kwamba ni muhimu kuliko wengine, yeye mtu yeyote akihitaji kuonana naye anaonana naye, ni watu wachache sana wenye moyo kama huo.

“Kwa hiyo kuhusu kauli yake kwamba hataki ubunge, mimi niseme kwamba hajawatendea haki wananchi wa Tarime. Yeye anaweza akasema hataki, lakini wananchi huku Tarime wanamhitaji. Kwa mfano mimi binafsi nikikuta imetokea kwamba anarudi, nitakuwa mstari wa mbele kushawishi watu kumuunga mkono,” alisema Ambrose.

Mwananchi mwingine mkazi wa kata ya Ganyange, Nashon Marwa aliyewahi kuwa diwani wa kata hiyo, alisema Nyambari bado anahitajika Tarime kwa sababu pia ni mtu ambaye si muumini wa makundi ndani na nje ya chama.

“Nyambari ni mtu ambaye hata baada ya kutoka madarakani hakuonekana kuwa kwenye kundi lolote, siku zote yeye ni mtu wa kusimama katikati. Lakini pia Nyambari ni mtu ambaye si tapeli, na alipokuwa mbunge hakujiingiza kwenye makundi ya rushwa na vile vile si mbaguzi wa koo.

“Nyambari aliunganisha wana-Tarime, na alisimama kidete kuhakikisha ubadhirifu haufanyiki katika halmashauri yetu, na ikumbukwe pia kwamba ndiye mbunge pekee aliyeleta shehena kubwa ya mabati kutoka TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) - akagawia wananchi hadharani kwenye uwanja wa Shamba la Bibi mjini Tarime.

“Lakini pia Nyambari ndiye alifanya wazazi wakaacha kununua vitabu kwa ajili ya watoto wao, maana alipeleka msaada wa vitabu kwenye shule za sekondari na msingi katika jimbo zima, na mpaka sasa ndiye aliyeongoza harambee nyingi akiwa mbunge, na hata nje ya ubunge tunaona anarudi kuongoza harambee za kuchangia maendeleo.

“Kikubwa zaidi, wana-Tarime watamkumbuka na kumthamini sana Nyambari kutokana na juhudi kubwa alizofanya kuondoa ubaguzi wa kikoo. Alifanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba mapigano ya kikoo hayaendelei tena. Kwa hiyo viongozi waliokuja wamekuta Tarime imeshatengenezwa na Nyambari.

“Barabara nyingi katika wilaya ya Tarime zilitengenezwa na kufunguliwa kipindi cha uongozi wa Nyambari. Kwa ujumla huyu ndugu ni mtu wa maendeleo, ni mtu asiye na makuu, chuki wala ubinafsi, ni mtu muhimu anayehitajika sana kwa Tarime ya sasa,” alisema Nashon.

Naye mkazi wa kata ya Matongo aliyejitambulisha kwa jina moja la Bhoke, akizungumza kwa lugha ya asili alisema kwa kifupi: “Nyambari Nyangwine alikuwa chachu ya maendeleo ya wananchi wa Tarime, hasa sisi wanawake, ila watu wachache walimhujumu tu kwa sababu ya maslahi na tamaa zao binafsi.”

Aidha, kwa upande wa mitandao ya kijamii, watu mbalimbali waliandika maoni yao juu ya kitendo cha Nyambari cha kuchangisha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga wiki iliyopita. Yafuatayo ni baadhi ya maoni yaliyotolewa na watu tofauti:

“Huyu [Nyambari] anakumbuka hata kuna Mungu.” “Mimi na familia yangu kuna mkono wa Nyambari, lakini pia kupitia kwake na madiwani wakati huo waliweza kulipia nusu ya ada kwa wanafunzi waliosoma shule za kata na boarding.” “Mbunge wetu wa zamani abarikiwe.”
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages