NEWS

Friday 15 December 2023

Tanzania yalikaribisha Bunge la Umoja wa Ulaya kukagua Ngorongoro




SIKU moja baada ya Bunge la Umoja wa Ulaya kulaani kuhamishwa jamii za watu wanaoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali ya Tanzania imetoa wito kwa Bunge hilo kwenda kukagua eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi, inaeleza kuwa Tanzania inalikaribisha Bunge la Ulaya kwani “Serikali haina kitu cha kuficha na inahakikisha wakati wote haki za binadamu zinaheshimiwa.”

Kwa upande mwingine, Matinyi ameweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania inatambua kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), litapeleka wataalamu wake Januari 2024 kufanya ukaguzi.

Tanzania imeendelea kukanusha madai ya kuhamishwa jamii hizo kwa nguvu, ikisisitiza kuwa wanahama kwa hiari kwenda katika maeneo ambayo Serikali imewajengea miundombinu yote muhimu.

Msemaji wa huyo wa Serikali ameongeza kuwa Tanzania haikaliwi kutokana na makabila ya watu.

“Eneo la Ngorongoro lina makabila zaidi ya moja na Serikali haitambui watu wake kwa makabila, na kila mtu wa kabila lolote nchini ana haki ya kuishi popote nchini. Kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu, hakuna kabila au kundi la watu lenye hadhi ya “watu wa asili” (indigenous people), bali watu wote ni sawa na huishi popote katika nchi ya Tanzania.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages