NEWS

Monday 4 December 2023

Wadau wa MVIWANYA waiomba Serikali kuimarisha usimamizi wa utekelezaji mipango ya kuboresha kilimo




Na Mwandishi wa Mara
Online News, Tarime
------------------------------


Serikali imeombwa kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango yake inayolenga kuwasaidia wakulima na kuinua sekta ya kilimo nchini.

Rai hiyo ilisisitizwa katika kikao cha Jukwaa la Wadau wa Kilimo na Watunga Sera kilichofanyika jana Tarime mkoani Mara, ambacho kiliandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA).


Kikao hicho kilikuwa cha kuwajulisha wadau hao matokeo ya maoni ya wakulima wadogo kuhusu sera, miongozo, masuala ya kiprogramu na changamoto zinazowakabili wakulima wadogo katika mikoa ya Kagera na Mara.

“Tunaomba Serikali isimamie utekelezaji wa mipango inayokuwa imeahidi kwa wakulima, ikiwmo ya kuwafikishia mbolea ya ruzuku kwa wakati, na ihimize maofisa ugani kuwatembelea wakulima mashambani kuwapa ushauri wa kitaalamu juu ya kilimo mseto kilicho bora na endelevu, ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Tarime (JUWATA), Gabriel Mwinga.


Mwinga akizungumza katika kikao hicho

Kwa upande wake Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava aliiomba Serikali kujiimarisha pia katika eneo la kusikiliza, kupokea na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha yao na kuchangia pato la taifa.

“Wakulima kutoshirikishwa katika vikao vya mipango na bajeti, ushuru na tozo kwenye mazao ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo, mikopo ya kusaidia kilimo, huduma za ugani pamoja na masoko ya uhakika ya mazao ni changamoto zinazodidimiza mkulima,” alisema Nguvava.


Nguvava akizungumza kikaoni

Naye mkulima na mwanachama wa JUWATA, Laurent Manga aliidokeza Mara Online News nje ya kikao hicho kwamba “kinachotolewa na Serikali kwa ajili ya mkulima hakimfikii kikamilifu, lakini pia Serikali hiyo hiyo haifuatilii kuona kama kimemfikia mkulima”.

Manga alitoa angalizo kwa Serikali kuongeza nguvu kwenye kilimo cha mahindi ili pia kuwezesha upatikanaji wa takwimu za uzalishaji wa zao hilo ambalo wakulima wengi wanalipatia kipaumbele.


Manga akidokeza jambo

“Nchi jirani ya Kenya ndiyo inayofaidi mahindi yetu kwa kununua tani nyingi, kisha wanatuuzia kwa bei ya juu. Kiundwe chombo kama cha WAMACU (Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara) kitakachosaidia kusimamia kilimo cha mahindi,” alisema Manga.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages