NEWS

Monday, 18 December 2023

Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara wakagua utekelezaji wa miradi wilayani Tarime




Na Christopher Gamaina
Mwandishi - Mara Online News
-------------------------------------------


WAJUMBE wa Bodi ya Barabara Mkoa wad Mara leo Jumatatu wamekagua miradi mbalimbali ya barabara inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri za Mji na Wilaya ya Tarime.

Miradi waliyokagua na thamani yake ikiwa kwenye mabano ni ujenzi wa kalavati la Kikomori (milioni 61), daraja la Kinyambi (milioni 549) na barabara ya Mogabiri-Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25 (bilioni 34.662) inayojengwa kwa kiwango cha lami.


Licha ya kueleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, wajumbe hao wa Bodi ya Barabara wamewataka wakandarasi husika kuiharakisha ili ianze kunufaisha wananchi.

Aidha, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi hiyo.



Wamezipongeza pia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tarime kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya barabara katika wilaya hizo.

“Pongezi kwa TARURA na TANROADS, tumetembelea na kuona kazi kubwa inayofanyika. Watekelezaji wa miradi hii fanyeni kazi nzuri ili mheshimishe wakandarasi wazawa,” amesema Daniel Komote ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.



Hata hivyo, wajumbe hao wa Bodi ya Barabara wameiomba Serikali kutochelewesha malipo ya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ili kuepusha visingizio vya kushindwa kuikamilisha kwa wakati.

“Mkandarasi akicheleweshewa malipo maana yake hata vijana wanaofanya vibarua kwenye miradi hii watacheleweshewa malipo, na miradi haitakamilika kwa wakati,” amesema mmoja wa wajumbe hao.



Wajumbe wengine wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara walioshiriki ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi ni pamoja na Mordikae Mseti ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakandarasi Mkoani humo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles.

Wajumbe hao wamefuatana na Meneja wa TARURA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa, mwakilishi wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Fraterh Shirima na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye aliyeongoza msafara huo wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya barabara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages