(Picha ya maktaba)
INDIA imetuma Jeshi lake la Wanamaji kuwasaidia wafanyakazi wa meli yake inayosemekana kutekwa na maharamia katika pwani ya Somalia.
Ripoti za vyombo vya habari vya India zinasema meli hiyo ina wafanyakazi 15 wa India.
Wafanyakazi hao waliomba msaada wa dharura kwa Shirika la Uendeshaji Biashara ya Baharini la Uingereza (UKMTO), wakisema "watu watano hadi sita wasio na kibali" walikuwa wamepanda meli hiyo mashariki mwa mji wa bandari wa Eyl, jana Alhamisi jioni.
Awali, wafanyakazi hao walikuwa wameiambia UKMTO kuwa wamejificha kwenye sehemu maalum ya meli hiyo - inayotumiwa kujilinda wakati wa dharura au vitisho vinapoweza kutokea kama vile uharamia.
Ndege ya doria "imeanzisha mawasiliano na chombo hicho, kubaini usalama wa wafanyakazi," Jeshi la Wanamaji limesema.
Meli ya INS Chennai "inakaribia [kufikia] chombo hicho ili kutoa usaidizi huku ndege ya wanamaji ikifuatilia meli hiyo, Jeshi la Wanamaji limeongeza.
Meli hiyo iliyopewa jina la MV Lila Norfolk na ambayo ina bendera ya Liberia, ilikuwa ikielekea Bahrain kabla ya kudaiwa kutekwa na maharamia.
Mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya meli katika pwani ya Somalia yamezua wasiwasi kwamba uharamia unaweza kurejea tena katika eneo hilo.
Mashambulizi ya maharamia, ambayo yalianza kutoka Eyl, yalikuwa changamoto kubwa kwa meli za kimataifa kutoka mwaka 2008 hadi 2011, katika hatua ambayo ilifanya mataifa kote duniani kutuma meli za kivita kufanya doria katika eneo hilo.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment