NEWS

Tuesday 2 January 2024

Nyambari atunukiwa Tuzo ya Heshima kwa Kukuza Kiswahili dunianiMke wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete (kulia), akimkabidhi Mwenyekiti wa NNGCL, Nyambari Nyangwine Tuzo ya Heshima wakati wa Tamasha la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro jana.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi wa Mara
Online News, Morogoro
-------------------------------


MCHAPISHAJI na msambazaji maarufu wa vitabu vya kiada na ziada vya shule za sekondari na msingi, Nyambari Nyangwine, ametunukiwa Tuzo ya Heshima kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Nyambari ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd (NNGCL), ametunukiwa Tuzo hiyo kwa heshima ya Shaaban Robert aliyekuwa Mwandishi, Mtunzi wa Insha na Mshairi maarufu kutoka Tanzania.

Shaaban Rbobert alikuwa Gwiji wa Fasihi ya Kiswahili ambaye aliandika vitabu vya riwaya, mashairi na insha mbalimbali wakati wa Ukoloni, na mpaka sasa vitabu vyake vilivyokwishachapishwa ni 24.
Nyambari Nyangwine
Nyambari alikabidhiwa Tuzo hiyo ya Heshima wakati wa Tamasha la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili na Kumbukizi ya Shaaban Robert lililofanyika Januari 1, 2024 katika Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), mgeni rasmi akiwa Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete..

Tuzo hiyo ya Heshima hutolewa kwa watu maarufu hasa Maprofesa wa Fasihi ya Kiswahili, ambapo Nyambari amekuwa miongoni mwa watu walioipata kabla ya kufikia hatua ya uprofesa.

Tuzo hiyo ni ya pili kwa Nyambari Nyangwine, kwani mwaka jana alitunukiwa Tuzo ya Heshima ya Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) kutambua mchango wake katika kukuza na kueneza Ushairi na lugha ya Kiswahili.


Kulia ni tuzo ambayo Nyambari alitunukiwa juzi na kushoto ni aliyotunukiwa mwaka jana.

Kwa upande mwingine, Nyambari alipongezwa kutokana na michango mikubwa ambayo amekuwa akitoa kusaidia na kudhamini programu, miradi na makongamano mbalimbali, pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi katika Fasihi ya Kiswahili, miongoni mwa masomo mengine.

Ilieleza katika tamasha hilo pia kwamba huduma ya Nyambari ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada na ziada imesaidia kwa kiwango kikubwa kukuza taaluma kwa wanafunzi waliovisoma.


Nyambari (kulia) akizungumza wakati wa tamasha hilo.
Watu mbalimbali, hasa vijana waliosoma vitabu hivyo walifunguka kwa kumshangilia Nyambari na kutoa ushuhuda mbele ya mgeni rasmi jinsi vilivyowasaidia kufikia malengo yao ya kielimu.

“Kushangiliwa na kupigiwa makofi mengi ni ushahidi kuwa vitabu vyako [Nyambari] vimewasaidia vijana hawa kufika hapo walipo na nafasi walizo nazo,” alisema mmoja wa washereheshaji wa tamasha hilo.

Tamasha hilo la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili na Kumbukizi ya Shaaban Robert ambalo lilidhaminiwa na NNGCL, lilihudhuria na viongozi na watu maarufu kutoka ndani na nje ya Tanzania, zikiwemo nchi za Ujerumani na Oman.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages