NEWS

Monday 26 February 2024

DC Mntejele awaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ziara ya Waziri Mkuu wilayani Tarime



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, 
Kanali Michael Mntenjele.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------


MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Kanali Michael Mntenjele ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa itakayofanyika wilayani humo kuanzia kesho Jumanne.

DC Mntenjele ametoa wito huo katika mkutano na vyombo vya habari ofisini kwake leo jioni, ambapo pia ameviomba vyombo vya habari kusaidia kuwafahamisha wananchi juu ya ziara hiyo, itakayohusisha uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na mikutano ya hadhara.

“Kwa kutumia media zenu (vyombo vya habari) mtasaidia kuwatangazia wananchi wajitokeze na hasa kwenye maeneo ya mikutano ya hadhara - kwa maana ya hapa Tarime mjini kwenye uwanja wa Serengeti na Sirari kwenye uwanja wa Tarafa, ili waweze kumsikiliza mheshimiwa Waziri Mkuu,” amewambia waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa DC Mntenjele, Waziri Mkuu Majaliwa atawasili wilayani Tarime kesho Jumanne [Februari 27, 2024] majira ya alasiri akitokea wilayani Serengeti na kupokewa Nyamwaga ambapo atasalimia wananchi na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya, kabla ya kuelekea mjini Tarime kupumzika.

Amesema kesho kutwa Jumatano [Februari 28, 2024], Waziri Mkuu ataelekea wilayani Rorya, kisha kurudi Tarime na kwenda Sirari kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Tarafa, na baadaye atarudi mjini Tarime kuweka jiwe la msingi katika soko kuu linalojengwa, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Serengeti.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages