Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (kushoto) akifurahi mara baada ya kukata utepe kuzindua kiwanda cha kuchakata kahawa cha WAMACU Ltd mjini Tarime jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya ushirika huo, David Hechei.
---------------------------------------------------
Mara Online News, Tarime
--------------------------------------
MKUU wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda amezindua kiwanda cha kuchakata kahawa cha Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU) Ltd, na kueleza kuridhishwa na utendaji wa menejimenti ya ushirika huo.
“Menejimenti nimeiona ina mwelekeo mzuri wa kuchapa kazi,” alisema Mtanda wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 14 wa Mwaka wa WAMACU Ltd, baada ya kuzindua kiwanda hicho mjini Tarime jana Januari 31, 2024.
Aliupongeza ushirika huo kwa kuanzisha kiwanda hicho chenye mashine za kisasa. “Kiwanda nimekikagua ni kizuri sana, endeleeni kuongeza mashine kulingana na mahitaji,” alisema.
Ukaguzi wa mitambo ya kiwanda
--------------------------------------------
Kwa upande mwingine, Mtanda aliipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuipatia WAMACU Ltd mkopo wa kuendesha shughuli zake zenye tija kwa wakulima.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito wa kuhamasisha wakulima kuchangamkia fursa ya mikopo, ikiwemo ya zana za kilimo kama vile matrekta - inayotolewa na TADB.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wataalamu wa kilimo na ushirika wa WAMACU Ltd na halmashauri za mkoa wa Mara kushirikiana katika kuimarisha shughuli za ugani kwa wakulima ili waweze kulima kwa tija.
Aliendelea kuhamasisha wananchi kutumia njia ya kilimo kujikwamua kiuchumi na kijamii, akisema matajiri wakubwa katika nchi zilizoendelea ni wale waliowekeza kwenye kilimo.
Sambamba na hilo, Mtanda aliwataka maofisa ugani kuhakikisha wanatoka ofisini Kwenda kuwahudumia wakulima mashambani, huku na wao wakiwa wakulima wa mfano.
“Tutakuwa tunatembelea mashamba yenu [maofisa ugani] kabla ya wakulima wengine, kwa sababu kuongoza lazima kuwe kwa vitendo, siyo maneno,” alisema.
Mkuu wa Mkoa, Said Mohamed Mtanda akihutubia mkutano huo.
------------------------------------------
Kuhusu maeneo ya WAMACU Ltd na vyama wanachama yaliyovamiwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali, Mtanda alielekeza taarifa hizo zifikishwe kwenye mamlaka husika kwa hatua za ufumbuzi ili kuepusha migogoro inayodumaza maendeleo ya sekta ya ushirika mkoani Mara.
Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye alisema ushirika huo ni muungano wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) vipatavyo 46, vinavyounganisha wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao, hususan kahawa na tumbaku kutoka maeneo ya wilaya za Tarime, Serengeti, Butiama, Rorya na Buchosa.
Alisema ushirika huo unamiliki raslimali mbalimbali, zikiwemo ardhi, majengo, maghala na mitambo - zenye thamani ya shilingi bilioni 4.223 zinazouwezesha kuingia mikataba na taasisi za fedha ili kupata mitaji ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za ukusanyaji, uchakataji na utafutaji wa masoko ya mazao yenye tija, kwa manufaa ya wanachama na wakulima.
Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye akisoma risara ya ushirika huo kwa mgeni rasmi.
----------------------------------------------
Aidha, Gisiboye alisema WAMACU Ltd kwa ushirikiano na TADB wameweza kugawa miche bora ya kahawa ipatayo 100,000 yenye thamani ya shilingi milioni 120.
Pia wameweza kutoa huduma ya pembejeo za kilimo, hasa mbolea na mbegu za mahindi zenye thamani ya shilingi bilioni 3.816 na kununua na kusimika mashine kubwa ya kuchakata kahawa mbivu na kavu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.303.
Mtanda akipanda mti wa kumbukumbu ndani ya eneo la makao makuu ya ofisi za WAMACU Ltd
-------------------------------------------------
Gisiboye aliongeza kuwa WAMACU Ltd kwa kushirikiana na TCDC na COASCO wameweza kutoa mafunzo kwa viongozi na watendaji 207 wa AMCOS mkoani Mara kwa gharama ya shilingi milioni 19.“Chama kimeweza kununua vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 20 ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli zake na kimethaminisha mali zote za ex-Mara Cooperative tulizokabidhi na za vyama wanachama zenye thamani ya shilingi bilioni 2.557 kwa thamani ya shilingi bilioni 1.442.
“Katika msimu wa 2021/2022, chama kiliweza kulipa wakulima malipo ya pili ya shilingi milioni 34.296 ambapo kilo moja ililipwa shilingi 200 na pia katika msimu wa 2020/2021, chama kililipa malipo ya pili kwa wakulima yenye thamani ya shilingi milioni 113 kwa bei ya shilingi 400 kwa kilo,” aliongeza Meneja Mkuu huyo wa WAMACU Ltd.
Mafanikio hayo ni matunda ya Bodi ya WAMACU Ltd chini ya Mwenyekiti wake, David Hechei, ambayo imeonesha umahiri katika kusimamia dhima ya kuratibu na kuunganisha AMCOS kwa ajili ya kukusanya, kuhifadhi, kuchakata, kutafuta masoko na kuuza mazao kwa tija.
Mkuu wa Mkoa, Saidi Mohamed Mtanda (wa pili kulia) akikabidhi cheti cha pongezi kwa kiongozi kwa AMCOS iliyofanya vizuri. Wa tatu ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, David Hechei.
-----------------------------------------------
Gisiboye alitaja matarajio ya ushirika huo kuwa ni kuhakikisha huduma ya pembejeo za kilimo inawafikia wakulima kwa wakati na kwa umbali usiozidi kilometa 10, kuanza huduma ya ukusanyaji wa mahindi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ndani, na kuendelea kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kahawa.
Matarajio mengine alisema ni kubuni miradi mipya itakayouongezea ushirika huo mapato kwa lengo la kuinua uchumi wake na kuimarisha kipato cha mkulima na kujiunga na ithbati mbalimbali za kimataifa zinazowezesha kufikia masoko ya kimataifa na yenye bei mzuri.
Lakini pia kuimarisha utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wakulima, viongozi na watendaji ili kuongeza uzalishaji wenye tija, kuimarisha utendaji na kuimarisha utawala bora (uwazi/ukweli na uwajibikaji), alisema Gisiboye.
No comments:
Post a Comment