NEWS

Thursday 15 February 2024

Kituo cha Haki za Binadamu Chuo Kikuu SAUT chalitaka Jeshi la Polisi Tarime Rorya kutoa taarifa ya mauaji ya kijana NyamwagaWakili Moses Matiko Misiwa
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
------------------------------------------


KITUO cha Haki za Binadamu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Mwanza, kimelaani tukio la mauaji ya kijana Jack Nyamonge, mkazi wa kijiji cha Nyamwaga, wilaya ya Tarime mkoani Mara, na kulitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa kwa umma.

“Kama Kituo cha Haki za Binadamu cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa kijana anayeitwa Jackson Nyamonge, mkazi wa kijiji cha Nyamwaga.

“Taarifa ya kifo inaonesha ameuawa siyo kifo cha asili, ni vema Jeshi la Polisi likatoa taarifa kuhusu kifo hicho,” amesema Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu cha SAUT Mwanza, Wakili Moses Matiko Misiwa katika taarifa aliyoitoa leo.

Aidha, kupitia taarifa hiyo, Wakili Misiwa ametishia kuwa kituo chake kitachukua hatua za kufanya uchunguzi wa kibinasi juu ya mauaji hayo, kama Jeshi la Polisi halitawajibike kutoa taarifa kwa umma.

“Kwa hiyo ni vyema Jeshi la Polisi likatoa taarifa za kiuchunguzi kutueleza sisi wananchi na kuieleza Serikali kuwa hicho wala hakihusiani na mgodi [akimaanisha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara] na ilihali wao ndio walikuwa wanamtafuta… maana taarifa ya hospitali inaonesha ameuawa.

“Wasipofanya hivyo, sisi tutachukua hatua za kiuchunguzi binafsi kwa sababu sheria inaruhusu na tutaijulisha Serikali,” amesema Wakili Misiwa katika taarifa yake.

Taarifa zilizopo zinaonesha Jack alikuwa kwenye orodha ya watu 21 waliokuwa wakitafutwa na Jeshi la Polisi kwa kutuhuma za kujihusha na vitendo mbalimbali za kihalifu.

Katika orodha hiyo ambayo ilisainiwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Nyamongo mnamo Oktoba 30, 2023, Jack alikuwa namba 17.

Mwili wa kijana huyo ulizikwa jana kijijini Nyamwaga, kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Juhudi za Mara Online News kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Tarime Rorya, Mark Njera kwa ajili ya kuzungumia tukio hilo hazijafanikiwa baada ya simu yake ambayo imekuwa ikiita bila kupokewa.

Hata hivyo, juhudi za kumpata RPC Njera bado zinaendelea.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages