NEWS

Friday 16 February 2024

RPC Tarime Rorya: Tunaendelea kuchunguza kifo cha Jackson NyamongeRPC Tarime Rorya, ACP Mark Njera.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------

JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya limesema litatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi wa kifo cha Jackson Nyamonge (28), mkazi wa kijiji cha Nyamwaga.

Akitoa taarifa ya tukio hilo katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mark Njera alisema mwili wa kijana huyo uliokotwa na askari polisi Februari 12, mwaka huu usiku, ukiwa umetelekezwa pembezoni mwa uzio wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo, kilomita chache kutoka kijijini Nyamwaga.

“Alikutwa akiwa na majeraha kichwani na tumboni yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali,” alisema ACP Njera.

Aidha, alisema uchunguzi walioufanya kupitia CCTV umebaini kuwa usiku huo huo watu 11 wanaosadikiwa kuwa wahalifu walivunja uzio na kuvamia mgodi huo wakiwa na silaha za jadi zikiwemo panga.

“Mmoja kati ya hao alionekana kudondoka ghafla, wenzake kwa haraka walimbeba na kukimbia kusikojulikana. Lakini baada ya saa moja walirudi na huyo mtu na kumtelekeza pembezoni mwa uzio wa mgodi huo.

“Watu hao waliharibu vibanda vya walinzi shirikishi katika mgodi huo na kujeruhi baadhi yao. Wakati uhalifu huu unafanyika haioneshi uwepo wa askari polisi katika eneo hilo.

“Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kifo cha Jackson kimesababishwa na kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha aliyopata,” alisema Kamanda Njera.

Jana kabla ya taarifa hiyo ya RPC Njera, Kituo cha Haki za Binadamu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Mwanza, kilizungumzia kifo cha Jackson Nyamonge na kutishia kufanya uchunguzi wa kibinafsi endapo Polisi wangeendelea kukaa kimya bila kutoa taarifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages