NEWS

Wednesday 14 February 2024

Benki ya Azania, Shirika la Nyumba Zanzibar wazindua mikopo ya nyumba za gharama nafuu




Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
-----------------------------------------


BENKI ya Azania kwa kushirikana na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), leo limezindua huduma ya mikopo ya nyumba zilizojengwa na shirika hilo katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba.

Hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo imefanyika katika Benki ya Azania Tawi la Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na utiaji saini makubaliano baina ya Benki ya Azania na ZHC, Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi wa benki hiyo, Jackson Lohay amesema kuwa benki imejipanga na iko tayari kuwakopesha watakaohitaji nyumba hizo ambazo gharama zake ni nafuu.

“Kwanza kabisa niwapongeze ZHC kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na sisi [Benki ya Azania], katika hili wameonesha uhalisia wa kuwa ni shirika ambalo linalenga kumuinua Mzanzibari kwa vitendo,” amesema Lohay na kuongeza kuwa Azania ndiyo benki ya kwanza nchini Tanzania kukopesha mikopo ya nyumba.

“Sisi Benki ya Azania tuko tayari kuwahudumia kwani hatuna ugeni kwenye biashara hii, tuna uzoefu wa kutosha kama ambavyo nimeeleza na tutawakopesha kwa riba ya chini sana - ya kuanzia asilimia 14 (reducing) tu, ambapo muda wa marejesho ni mpaka kufikia miaka 25 na masharti yake ni nafuu sana. Mtanzania yeyote anaruhusiwa - ilimradi awe anakidhi vigezo na masharti ya kuweza kurejesha kulingana na mtiririko wa malipo,” amesema Lohay.



Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa AZC, Mwanaisha Ali Said amesema makubaliano waliyoingia na Benki ya Azania yatawapa urahisi zaidi wateja wao kwani sasa watakuwa na wigo mpana wa kuwawezesha kununua na kumiliki nyumba bila hofu.

‘’Kuingia kwa makubaliano haya ni muendelezo wa mipango yetu kama shirika - ya kuwawezesha Wazanzibari kununua nyumba kwa njia rahisi, nyumba zetu huwa tunaziuza kwa njia kadhaa ikiwemo fedha taslimu na pia kwa njia ya mkopo, yaani Mortgage, baada ya kuona ununuzi kwa njia ya mkopo hatujafanya vizuri sana ndipo tuliwafuata Benki ya Azania kwa kuwa tunafahamu wao wana uzoefu mkubwa katika eneo hilo la Mortgage Financing na hatimaye leo tunatiliana saini makubaliano rasmi.

“Niwasihi wananchi wote kuchangamkia fursa hii, kwa sasa tuna mradi wa eneo la Mombasa kwa Mchina hapa Zanzibar wa ujenzi wa nyumba 72 ambapo takriban asilimia 90 zimeshanunuliwa, lakini pia kuna miradi mingine kama wa eneo la Mfikiwa, Chakechake kule Pemba nyumba 220, Nyamanzi hapa Zanzibar nyumba 120 na Kisakakasaka nyumba 240,” amesema Mwanaisha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages