NEWS

Friday 9 February 2024

DC Mashinji: Serikali imetoa trilioni 2/- kubadilisha mji wa Mugumu kuwa Serengeti Smart CityTaswira ya sasa ya mji wa Mugumu
------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Serengeti
----------------------------------------


MKUU wa Wilaya (DC) ya Serengeti mkoani Mara, Dkt Vincent Mashinji amesema Serikali imetoa shilingi zaidi ya trilioni mbili kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa miundombinu itakayoubadilisha mji wa Mugumu kuwa wa kisasa - utakaojulikana kwa jina la Serengeti Smart City.

DC Mashinji alitangaza hilo mjini Mugumu jana Februari 8, 2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, ambacho kilipokea na kukubali mradi huo.


Madiwani kikaoni
---------------------------
Mradi huo unaolenga kubadilisha taswira ya wilaya hiyo ambayo eneo lake kubwa ni Hifadhi ya Taifa Serengeti, utahusisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Serengeti hadi Mwanza, uboreshaji wa huduma za kijamii na miradi iliyokwama miaka mingi, ikiwemo uwanja wa ndege.

“Tulianzisha andiko la mradi wa Serengeti Smart City, Serikali imekubali, tayari zaidi ya trilioni mbili zipo tayari kujenga mji wa kisasa Serengeti, utakuwa ni mradi shirikishi kati ya Serikali na wananchi,” alisema Dkt Mashinji.

Aliongeza: “Tayari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti [Afraha Hassan] ameitwa Dodoma kwenda kujadili ujenzi wa uwanja wa ndege Serengeti, na asilimia 30 ya fedha hizo [za ujenzi] zitaenda kwenye kampuni za wazawa.”


Dkt Vincent Mashinji akitangaza mradi huo
-------------------------------------------
Naye Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya hiyo, Ayub Mwita Makuruma alisema ujenzi wa mji wa kisasa [Serengeti Smart City] utachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya hiyo.

“Ardhi itapanda thamani, kutakuwa na barabara na hospitali bora, mapato yataongezeka kutokana na utalii, na mambo mengine mengi,” alisema Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kwa tiketi ya chama tawala - CCM.


Makuruma akizungumza kikaoni
-------------------------------------------
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Mrobanda Japan Mkome aliwahimiza madiwani kushirikiana katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ili kupunguza malalamiko.

“Hatutaki kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kukiwa na malalamiko ya wananchi, simamieni ilani ya uchaguzi kwa weledi,” alisisitiza.


Mrobanda Japan Mkome
-----------------------------------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages