NEWS

Thursday 1 February 2024

TANAPA wakabidhi miradi ya kijamii kwa RC Mara katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Serengeti Tarime VijijiniMkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (katikati nyuma) akifurahia picha ya pamoja na wananchi wakati wa makabidhiano ya miradi ya kijamii iliyofadhiliwa na TANAPA katika kata za Nyanungu na Kwihancha wilayani Tarime jana.
----------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Tarime
-------------------------------------


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekabidhi vyumba vitatu vya madarasa na madawati 60 katika Shule ya Msingi Kegonga iliyopo kata ya Nyanungu, pamoja na nyumba ya walimu (pacha tatu) katika Shule ya Msingi Byantang'ana iliyopo kata ya Kwihancha, zinazopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini], mkoani Mara.

TANAPA ilikabidhi miradi hiyo ya elimu kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda, katika hafla mbili fupi zilizofanyika kwa nyakati tofauti, ambazo zilihudhuriwa pia na wananchi na viongozi wa vijiji, kata na wilaya, jana Januari 1, 2024.


Sehemu ya mbele wa vyumba vipya vya madarasa vilivyojengwa katika Shule ya Msingi Kegonga.
----------------------------------------
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Moronda Moronda alisema miradi hiyo imefadhiliwa na TANAPA na kutekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambapo wananchi walichangia asilimia 10 ya gharama zilizotumika.


Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda akizungumza wakati wa makabidhiano ya miradi hiyo.
-------------------------------------------
Moronda alifafanua kuwa mradi wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa umegharimu shilingi zaidi ya milioni 71, na nyumba ya walimu imegharimu shilingi milioni 103.


Sehemu ya mbele ya nyumba mpya ya walimu (pacha tatu) iliyojengwa katika Shule ya Msingi Byantang'ana.
------------------------------------------
Aidha, Moronda alidokeza kuwa TANAPA ina mpango wa kufadhili miradi ya ujenzi wa mabwawa ya maji katika vijiji vya Kegonga na Masanga kwa gharama ya shilingi milioni 250 kila moja, pamoja ukarabati wa bwawa katika kijiji cha Gibaso, vilivyopo jirani na hifadhi ya Taifa Serengeti.

Akizungumza baada ya kukagua, kuzindua na kukabidhiwa miradi hiyo ya elimu kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Mkoa, Mtanda, aliishukuru TANAPA kwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa miundombinu ya sekta hiyo nchini.


Mkuu wa Mkoa akizindua mradi
-------------------------------------------
RC Mtanda aliwapongeza wananchi wa kata za Nyanungu na Kwihancha kwa kuchangia asilimia 10 ya gharama za ujenzi wa miradi hiyo na kuwaomba kuendelea na moyo huo wa utayari wa kuchangia maendeleo ya umma.

“Waswahili wanasema ukibebwa nawe jibebe. Uwekezaji katika elimu ni kitu muhimu sana, wazazi waliokosa elimu wasitamani watoto wao nao wakaikosa, hata kama ajira haitoshi - mtu akisoma anapata mwanga mkubwa wa kuelewa mambo,” alisema Mtanda.

Kiongozi huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuhimiza watumishi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na wananchi wa vijiji vinavyopakana nayo wilayani Tarime kuendelea kuimarisha uhusiano na ujirani mwema kwa maslahi ya pande zote mbili.Awali, akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kegonga, Moses Mkwalakwala aliishukuru TANAPA, akisema upatikanaji wa madarasa matatu na madawati 60 umeboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia shuleni hapo, na kwamba utapunguza msongamano wa wanafunzi wakati wa vipindi vya masomo.

TANAPA ina utaratibu wa kufadhili ujenzi na uboreshaji wa miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo jirani na Hifadhi za Taifa, ikiwemo Serengeti kwa dhumuni la kudumisha uhusiano na ujirani mwema na wanavijiji husika, ili nao waone umuhimu wa kushiriki katika uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori na mazingira kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages