NEWS

Monday 18 March 2024

Bonde la Mto Mara linavyonusuru maisha ya binadamu na viumbe hai Ziwa Victoria, WWF, wadau watathmini utekelezaji mradi wa uhifadhi wa dakio la mto huo



Muonekano wa sehemu 
ya Bonde la Mto Mara.
-------------------------------------------------------

NA CHRISTOPHER GAMAINA
----------------------------------------------


MTAFITI kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dkt Makarius Lalika amesema uhifadhi wa mazingira katika bonde la mto Mara ni muhimu kwa sababu lina mchango mkubwa katika kulinda afya na maisha ya binadamu na viumbe hai katika Ziwa Victoria.

Dkt Lalika aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada ya utafiti alioufanya kuhusu uhifadhi wa dakio la mto Mara, wakati wa kikao cha wadau wa uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kilichoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania, mjini Musoma wiki iliyopita.

“Uhifadhi wa mazingira katika bonde la mto Mara ni muhimu kwa sababu ya ikolojia yake… ni eneo ambalo linanyonya uchafu ambao kama lisingekuwepo, uchafu ule ungeenda moja kwa moja ziwani na kuathiri afya na maisha ya viumbe wa ziwani.

“Kwa hiyo kuwepo kwa bonde hili, hasa ardhi oevu ya bonde la mto Mara kunasaidia kuchuja maji na kunyonya uchafu ambao mwisho wa siku ungeweza kusababisha madhara ya kimazingira na kibinadamu kwa jamii zilipo chini ambazo zinanufaika na maji ya mto huu,” alisema Mhadhiri huyo kutoka SUA.


Dkt Lalika akiwasilisha mada kikaoni.
--------------------------------------------

Dkt Lalika alisema utafiti alioufanya uliangalia namna WWF Tanzania inavyoweza kuwahusisha watunzaji wa vyanzo vya maji na wanufaika wa utunzaji wa vyanzo vya maji katika bonde la mto huo.

“Kwa upande wa wahifadhi wa vyanzo vya maji, tuliangalia namna gani wanaweza kuendelea kuhifadhi mazingira, hasa vyanzo vya maji ili viendelee kutoa maji katika mtizamo endelevu.

“Kwa upande wa watu waliopo katika bonde la mto Mara, tulikuwa tunazungumza nao kuhusu namna gani wanaweza wakachangia uhifadhi wa vyanzo vya maji,” alisema Dkt Lalika.

Aliongeza: “Kwa ufupi ni kwamba tulikuwa tunaangalia namna gani wanaweza kuchangia sehemu kidogo ya pato wanalolipata kutokana na utumiaji wa maji ili liweze kwenda kwa wahifadhi wa vyanzo vya maji kama sehemu ya kuwatia moyo waendelee kuhifadhi vyanzo vya maji.”


Sehemu ya wadau wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara wakimfuatilia Dkt Makarius Lalika wakati akiwasilisha mada kikaoni mjini Musoma hivi karibuni.
----------------------------------------

Dkt Lalika alisema yeye na timu yake katika utafiti huo, waligundua kwamba watu walioko juu vilipo vyanzo vya maji wako tayari kuendelea kuhifadhi mazingira ili kusaidia mtiririko endelevu wa maji katika bonde la mto Mara.

Lakini kwa watu waliopo chini, alisema hajaonekana mnunuaji wa maji mkubwa anayejulikana, hivyo bado utafiti huo unaendelea ili kuweza kubaini watu wanaoweza kuhusishwa na WWF Tanzania katika utunzaji wa vyanzo vya maji vya mto huo.

“Utafiti huu au wasilisho hili ni la mwanzo tu, kwa hiyo hata mapendekezo yaliyotolewa ni ya mwanzo, baada ya kuchakata maoni ya watu tutaenda kuyaingiza kwenye andiko letu na kutoa maoni ya mwisho ya nini kifanyike,” alisema Dkt Lalika.

Hata hivyo, alisema mapendekezo ya mwanzo yanaonesha kwamba uhifadhi wa mazingira katika dakio la mto Mara haukwepeki kutokana na umuhimu wake kisayansi na kiikolojia, lakini pia kwa sababu ya mchango wa kiuchumi wa watu katika ngazi ya kaya.


Sehemu ya washiriki kikaoni.
--------------------------------------

WWF waonesha dalili njema 
za vyanzo vya maji endelevu
Kuna kila dalili kuwa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara unaotekelezwa na WWF Tanzania, utachochea na kuunganisha wadau katika juhudi za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa vyanzo vya maji ya mto huo.

Mradi huo ambao ni wa miaka mitatu inayoishia Aprili 2025, unafadhiliwa na USAID/ Tanzania, ukitekelezwa katika mkoa wa Mara unaoundwa na wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama and Musoma, nchini Tanzania.

Wiki iliyopita, WWF Tanzania iliwakutanisha wadau wa mradi huo katika kikao cha kupeana mrejesho wa utekelezwaji wa shughuli za mradi, kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2024 na kupendekeza njia sitahiki za kuboresha utekelezaji.

Kikao hicho cha siku mbili kilifanyika mjini Musoma, ambapo kilihudhuriwa na wadau kutoka Halmashauri za Wilaya, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Ofisi ya Afisa Tawala Mkoa, taasisi zisizo za kiserikali na jumuiya za watumia maji.


Washiriki wa kikao hicho 
katika picha ya pamoja.
------------------------------------------

Washiriki wengine walitoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), waandishi wa habari na WWF Tanzania.

Mratibu wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara, Mhandisi Christian Chonya aliwapitisha wadau hao kwenye mada inayoangazia malengo ya mradi huo.

Alisema taasisi za maji kwenye dakio la mto Mara zina uwezo wa kushiriki, kuratibu na kutekeleza usimamizi wa rasilimali za maji shirikishi, na kuwa na uendelevu wa usambazaji wa maji kwenye jamii kupitia uhifadhi wa rasilimali za maji kwenye dakio la mto Mara.

Lakini pia kuratibu mapendekezo ya mifumo bora ya malipo ili kuboresha uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa ajili ya uhakika wa upatikanaji maji na uhifadhi endelevu wa dakio la mto huo unaomwaga maji katika Ziwa Victoria.


Wahiriki wakimfuatilia Mhandisi Chonya wakati akiwasilisha mada kikaoni.
-------------------------------------------

Mhandisi Chonya alitaja lengo mahsusi la mradi huo kuwa ni kusaidia kutatua changamoto za usalama wa maji na kustahimili mabadiliko ya tabianchi yaliyopo na yanayoongezeka miongoni mwa jamii.

Alibainisha kuwa wanufaika wa mradi huo ni watu 20,000 kupitia uhifadhi wa vyanzo vya maji, 6,000 kupitia uboreshaji wa usambazaji wa maji, na 1,200 kupitia uboreshaji wa maisha ya watu.

Kisha washiriki wa kikao hicho walipewa nafasi ya kuwasilisha taarifa fupi za utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mazingira, hususan upandaji miti, utunzaji misitu na vyanzo vya maji katika maeneo yao ya uongozi, pamoja na majadiliano ya jumla.

Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Mafunzo kutoka WWF Tanzania, Enock Edward Rutaihwa alisema jukumu kubwa la shirika hilo ni kuhifadhi mazingira kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika eneo la mradi huo.


Enock akizungumza katika kikao hicho.
--------------------------------------------
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages