NEWS

Friday 8 March 2024

Fahamu chanzo na umuhimu wa Siku ya Wanawake Duniani




WATU duniani kote leo wanasherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake (International Women's Day - IWD) ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Lakini siku hii ilianza vipi,
na kwanini ni muhimu?
Siku ya Kimataifa ya Wanawake ilikuja kutokana na harakati za wafanyakazi. Mbegu hizo zilipandwa mwaka wa 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika jiji la New York, Marekani wakidai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.

Mwaka uliofuata, Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya kwanza.

Wazo la kuifanya siku hii kuwa tukio la kimataifa lilitoka kwa Clara Zetkin, mwanaharakati wa kikomunisti na mtetezi wa haki za wanawake.

Mwaka 1910, aliizungumzia siku hii kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake Wanaofanya Kazi huko Copenhagen. Pendekezo lake liliungwa mkono kwa kauli moja na wanawake 100 kutoka nchi 17 waliohudhuria mkutano huo.

Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake iliadhimishwa mwaka 1911 katika nchi za Austria, Denmark, Ujerumani na Uswizi.

Umoja wa Mataifa (UN) ulianza kuadhimisha siku hii mwaka 1975. Kaulimbiu ya kwanza iliyopitishwa na UN mwaka 1996 ilisema: "Kuadhimisha Yaliyopita, Kupanga kwa Ajili ya Baadaye."

Kwanini huadhimishwa
Machi 8 kila mwaka?
Wazo la asili la Clara Zetkin la sherehe ya kimataifa halikuhusishwa na siku fulani. Tarehe 8 Machi ilichaguliwa baada ya wanawake wa Urusi kudai "mkate na amani" wakati wa mgomo kipindi cha vita mwaka 1917. Siku nne baada ya mgomo huo, Mfalme alilazimika kujiuzulu, na serikali ya muda iliwapa wanawake haki ya kupiga kura.

Kulingana na kalenda ya Julian ambayo wakati huo ilikuwa ikitumika nchini Urusi, mgomo wa wanawake ulianza Februari 23. Katika kalenda ya Gregori inayotumika sehemu nyingi duniani, tarehe hiyo ni Machi 8.

Je, siku hii inaadhimishwa
katika mataifa yote duniani?
Siku ya Kimataifa ya Wanawake ni sikukuu ya kitaifa katika nchi nyingi. Nchini China wanawake wengi hupewa mapumziko ya nusu siku ya kazi.

Maelfu ya matukio yanafanyika duniani kote, yakiwemo maandamano, mazungumzo, matamasha, maonesho na mijadala.

Nchini Italia, siku hii inaitwa Festa della Donna, na maua ya mimosa ni zawadi maarufu. Maua nchini Urusi kwa kawaida huongezeka maradufu karibu na Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Nchini Marekani, Machi ni mwezi wa Historia ya Wanawake. Tangazo la rais linalotolewa kila mwaka linaheshimu mafanikio ya wanawake wa taifa hilo.

Katika chapisho la Instagram mwanzoni mwa Machi 2024, Rais wa Marekani, Joe Biden alisema mwezi huo "utasherehekea urithi wa waimbaji walioimbwa na ambao hawajaimbwa, na watetezi ambao wameifanya dunia kuwa ya haki, haki zaidi, na mahali huru".

Kwanini watu huvaa rangi
ya zambarau siku hii?
Zambarau, kijani na nyeupe ni rangi za siku hii, kulingana na tovuti ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Inasema kwamba: "Zambarau inaashiria haki na heshima. Kijani inaashiria matumaini. Nyeupe inawakilisha usafi, ingawa ni dhana yenye utata".

Je, mada ya siku hii
mwaka 2024 ni nini?
Kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2024 ni "Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii", ambayo inalenga kuangazia umuhimu wa hatua za usawa wa kijinsia.

"Migogoro na kupanda kwa bei kunaweza kusababisha asilimia 75 ya nchi kupunguza matumizi ya umma ifikapo mwaka 2025, na kuathiri vibaya wanawake na huduma zao muhimu," UN inaonya.

Tovuti ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake imechagua mada "Kuhamasisha Ushirikishwaji". Inasema waandaaji na matukio yanalenga "kuvunja vikwazo, kupinga dhana potofu na kuunda mazingira ambapo wanawake wote wanathaminiwa na kuheshimiwa."

Kwanini wanaharakati
wanathamini siku hii?
Waratibu wanasema siku hii inatoa fursa ya kuashiria maendeleo yaliyopatikana, lakini pia kuangazia mmomonyoko wa haki za wanawake duniani, pamoja na madhara ya unyanyasaji wa kijinsia.

Katika miezi 12 iliyopita, wanawake katika Mashariki ya Kati, Afghanistan, Iran na Ukraine wamekuwa wakipigania haki zao huku kukiwa na vita na vurugu.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema wamepokea madai ya kuaminika ya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wanawake na wasichana huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kesi za ubakaji na vikosi vya Israel.

BBC pia imeona ushahidi wa ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na ukeketaji wanawake wa Israeli wakati wa shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023.

Nchini Afghanistan, wasichana walio juu ya umri wa kwenda shule ya msingi wanasalia kupigwa marufuku kutoka madarasani na Taliban, na hivyo kuwazuia wanawake kupata elimu.

Nchini Iran, wengi wanaendelea kukiuka sheria zinazowataka wanawake kufunika nywele zao, huku wanaharakati kama vile mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Narges Mohammadi wanakabiliwa na kifungo cha muda mrefu jela.

Umoja wa Mataifa unasema wanawake na wasichana nchini Sudan wanatekwa nyara na kubakwa katika maeneo yanayodhibitiwa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), ambapo wanalazimishwa kuolewa na wanashikiliwa ili kulipwa kikombozi.

Kulingana na Kielezo cha Global la Jinsia Duniani cha mwaka 2023, kinachochapishwa kila mwaka na Jukwaa la Kiuchumi la Dunia, hakuna nchi ambayo bado imefikia usawa kamili wa kijinsia. Inaonya kuwa huenda ikachukua zaidi ya karne moja kabla ya kufikiwa kote ulimwenguni.

Je, kuna Siku
ya Wanaume?
Siku ya Kimataifa ya Wanaume hufanyika Novemba 19 kila mwaka tangu miaka ya 1990. Tukio hili halitambuliwi na Umoja wa Mataifa, lakini limeangaziwa katika nchi zai ya 80 duniani, ikiwemo Uingereza.

Siku hiyo inaangazia "thamani chanya ambayo wanaume huleta kwa ulimwengu, familia zao na jamii", kulingana na waandaaji. Inalenga kuangazia mifano chanya ya kuigwa, kuongeza ufahamu wa ustawi wa wanaume na kuboresha mahusiano ya kijinsia.

Kwa miaka mingi, mcheshi Richard Herring alichangisha maelfu ya pauni kwa shirika la unyanyasaji la nyumbani la Refuge kila Siku ya Kimataifa ya Wanawake, kwa kujibu watu kwenye X (zamani Twitter), ambao walikuwa na hasira kuhusu ukosefu wa Siku ya Kimataifa ya Wanaume. 
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages