NEWS

Thursday 7 March 2024

Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani: TALGWU Mara wapeleka misaada Hospitali ya Tarime Mji



Kamati ya Ushauri Wafanyakazi Wanawake - TALGWU Mkoa wa Mara wakikabishi msaada wa shuka kadhaa kwa ajili ya wagonjwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime jana.
----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


KAMATI ya Ushauri Wafanyakazi Wanawake - TALGWU Mkoa wa Mara imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuwajulia hali na kuwapatia wagonjwa waliolazwa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime misaada ya sabuni, shuka na madumu ya kuhifadhia taka.

Aidha, Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Neema Banagi imewakabidhi wauguzi wa wodi hiyo zawadi ya vitambaa vya kushona sare zao za kazi.


Wakikabidhi zawadi ya vitambaa vya sare za wauguzi.
-----------------------------------------
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi, Banagi amewaomba wauguzi kudumisha upendo na huruma kwa wagonjwa.

“Niwaombe watumishi mliopo hapa muendelee na moyo wa huruma kwa wagojwa wetu waweze kufarijika, huu ni mwezi wa Kwaresma, akina mama wajawazito wanapenda kubembelezwa hadi wanapojifungua, bila ujauzito hakuna watu, Mwenyezi Mungu awabariki,” amesema.


Walipata pia fursa ya kuwajulia hali wagonjwa wodini.
---------------------------------------
Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Veronica Mwita ameishukuru Kamati hiyo kwa kuonesha moyo wa upendo wa kupeleka misaada hiyo kwa wagonjwa na wauguzi.

“Tunaahidi sisi kama wanawake tutatenda mazuri kwa kuwahudumia akina mama kwa kauli yetu isemayo ‘mpe mama mtoto’. Kila mama anayekuja kupata huduma (kujifungua) lazima tumpe mtoto,” amesema Veronica.

Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages