NEWS

Tuesday 19 March 2024

Waitara, Lusinde wazuru Kituo cha Afya Genkuru Tarime Vijijini kilichojengwa kutokana na mamilioni ya fedha kutoka Barrick North Mara, mganga ataja vikwazo



Sehemu ya majengo ya 
Kituo cha Afya Genkuru.
--------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


WABUNGE Livingstone Lusinde wa Jimbo la Mtera mkoani Dodoma, na Mwita Waitara wa Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, jana walizuru katika Kituo cha Afya Genkuru na kuzitaka mamlaka husika kupeleka huduma za maji na umeme kituoni hapo.

“Tunapozungumzia maji tunazungumzia uhai wa watu, hivyo tunaomba maji na umeme viwahishwe visiwe vikwazo katika huduma za kituo hiki kwa wananchi,” alisema Mbunge Lusinde maarufu kwa jina la Kibajaji, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama tawala - CCM.


Waitara akisisitiza jambo akiwa na Lusinde katika mkutano wa hadhara kituoni hapo.
-------------------------------------------

Awali, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Genkuru, Toreza Mussa alisema mradi huo ulijengwa mwaka 2018 kutokana na shilingi milioni 925 zilitotolewa na mgodi wa North Mara, zikiwemo milioni 774 zilizotokana na gawio la asilimia moja na shilingi milioni 151 za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Aidha, shilingi milioni 11 kutoka CSR ya mwaka 2020/2021 ziliongezwa kwa ajili ya ujenzi wa kichomea taka (incinerator) na shimo la kutupa kondo la nyuma, lakini pia shilingi milioni 140 za CSR ya mwaka 2021/2022 ziliongezwa ili kugharimia ukamilishaji wa majengo,” alisema Toreza.

Alifafanua kuwa kituo hicho cha afya kina jengo la wagonjwa wa nje, wagonjwa wa ndani, wodi ya mama na mtoto, jengo la upasuaji, maabara, jengo la kuhifadhi maiti, nyumba pacha mbili ya watumishi na choo chenye matundu manne.

Aidha, alisema kwa sasa kituo hicho kina watumishi tisa na kwamba huduma zinazotolewa hapo ni za wagonjwa wa nje (OPD), wagonjwa wa ndani (IPD), kliniki (RCH), CTC, upasuaji, mama na mtoto na maabara.



Hata hivyo, Toreza alisema kituo hicho cha afya kinakabiliwa na upungufu wa watumishi 38, ukosefu wa maji, umeme na uzio.

Kutokana na hali hiyo, Mbunge Waitara aliwataka wataalamu kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na TANESCO Wilaya ya Tarime kutamka mbele ya mkutano huo ni lini watapeleka huduma za maji na umeme kituo hapo.

Kwa upande wake Mhandisi Mohamed Mtopa kutoka RUWASA alisema tayari wameshatenga shilingi milioni 997 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kituoni hapo, na kwamba mkandarasi husika anatarajiwa kuanza kazi hiyo wiki ijayo.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Tarime, Masimino Swalo yeye alisema ofisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa kituo hicho kinaunganishiwa huduma ya umeme kufikia mwanzoni mwa mwezi ujao.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuhakikisha huduma za kijamii zinaboreshwa.

“Kituo hiki [Genkuru] ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi), Serikali imetuletea waganga, kituo kinatoa huduma, tumeona dawa zipo wananchi hawana malalamiko kuhusu dawa, wanaendelea kupata huduma,” alisema Mwl Mwaisenye.


Mwl Mwaisenye akizungumza 
katika mkutano huo.
----------------------------------------

Pia DAS huyo aliipongeza Kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kwa kutoa mamilioni ya fedha yaliyofanikisha ujenzi wa kituo hicho. “Niwapongeze sana mgodi wa Barrick kwa kuhakikisha kituo hiki kinakamilika na kuendeleza huduma kwa wananchi,” alisema DAS huyo.

“Ninachoweza kuwaomba vijana wenzangu ni kuwalinda wawekezaji, tunaona faida za uwekezaji kama hizi za kusaidia ujenzi wa miradi ya kijamii. Tukiendelea kulinda wawekezaji wakazalisha vizuri tutapata matunda mengi zaidi,” alisisitiza Mwl Mwaisenye.

Mbali na DAS huyo, viongozi wengine waliofuatana na wabunge hao ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya, Samwel Mangalaya, Katibu wa UWT Wilaya, Nyasatu Manumbu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Wilaya, Marema Sollo na Afisa Tarafa ya Ingwe, James Yunge, miongoni mwa wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages