NEWS

Sunday 31 March 2024

Waziri Mkuu Majaliwa amwakilisha Rais Samia mazishi ya mke wa MNEC Gachuma wilayani TarimeMjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Christopher Mwita Gachuma (kulia) akimpokea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowasili nyumbani kwake kijijini Komaswa wilayani Tarime jana kuhudhuria hafla ya mazishi ya mke wa Gachuma, Francisca.
---------------------------------------------

Na Mana Online News, Tarime
------------------------------------------


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye hafla ya mazishi ya mke wa Christopher Mwita Gachuma, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Mheshimiwa Gachuma, watoto wa marehemu, ndugu na jamaa, pokeeni salamu za pole kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Msiba huu unatugusa pia sisi serikali, kwa sababu mama huyu alikuwa anatoa mchango mkubwa kumfanya Gachuma awe mstari wa mbele kwenye mipango yake,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati wa hafla ya mazishi ya marehemu Fransisca (74) nyumbani kwa Gachuma kijijini Komaswa jana Machi 30, 2024.


Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi (kushoto) akiteta jambo na MNEC Gachuma.
----------------------------------------------


Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt Rhimo Simeon Nyansaho (katikati) na waombolezaji wengine msibani hapo.
----------------------------------------------

Majaliwa alisema Rais Samia anafanya kazi na MNEC Gachuma kwa karibu na kwamba amekuwa na msaada mkubwa wa kimaendeleo serikalini.

“Mheshimiwa Gachuma tumefanya naye kazi ndani ya serikali akiwa si mtumishi, bali ni mdau wa kuiunga mkono serikali, amekuwa mshiriki mkubwa wa maendeleo kwenye sekta mbalimbali, zikiwemo za viwanda na kilimo, tunashukuru kwa mchango wake kwa serikali,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ibada ya mazishi hayo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la New Life Gospel Community (NLGCC), Dkt Daniel Ouma ambaye alisema mke wa Gachuma, Francisca, alikuwa Askofu wa Kanisa hilo Jimbo la Mara Kaskazini.


Waziri Mkuu Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa Francisca.
----------------------------------------------

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, Katibu wa NEC ya CCM Taifa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda (ameteuliwa na Rais Samia leo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha) na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, miongoni mwa wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages