NEWS

Monday 8 April 2024

AICT, Right to Play wapaisha mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni
NA JOSEPH MAUNYA, Serengeti
-------------------------------------------


KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play limetajwa kuchangia ongezeko la mahudhurio ya wanafunzi, hususan wa kike shuleni kutokana na uhamasishaji linaoufanya.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwl Amani Ndodo wa Shule ya Msingi Nyakitono iliyopo wilayani Serengeti, Mara wakati wa tamasha la michezo la uhamasishaji juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike lililoandaliwa na AICT kwa ushirikiano na Right to Play katika viwanja vya shule hiyo hivi karibuni.

“Kupitia matamasha haya tunaona mabadiliko mengi sana, kwa mfano mahudhurio yameongezeka sana, hasa hasa ya watoto wa kike tofauti na zamani. Lakini pia watoto wa kike wameongeza kujiamini na hawaogopi kuchangamana na wenzao kama zamani,” alisema Mwl Ndodo.


Mwanafunzi wa kike akiwakilisha wenzake kupokea kombe la ushindi kwenye tamasha hilo.
----------------------------------------------

Kwa upande wao, watoa mada kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Neema Kazimili Matonange na Felister John Ulanga walihimiza wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya kupata elimu.

“Na ninyi wanafunzi mkifika mitaani mkawaona wenzenu walioacha ama kuachishwa shule basi muwashauri waje shuleni ili nao wapate elimu kama ninyi, na kwa hali hiyo ninyi pia mtakuwa mmeshiriki uhamasishaji huu,” alisema Neema.

“Walimu na wazazi tunawaomba sana muwape msaada hawa watoto wetu wa kike ili wapate elimu iliyo bora, kusiwe na ubaguzi na badala yake tuwajenge vizuri kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi,” alisema Felister.

Naye Afisa Nradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisema lengo la mradi unaojulikana kama 'Save her sit' (Linda kiti cha mtoto wa kike) ni kuihamasisha jamii itambue umuhimu wa kumuelimisha mtoto wa kike, lakini pia kuwasaidia wale wanaoishi katika mazingira magumu kupata elimu iliyo bora kama wanafunzi wengine.


Daniel Fungo akizungumza 
katika tamasha hilo.
-------------------------------------------
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages