NEWS

Monday 8 April 2024

Mgodi wa Barrick North Mara unavyochochea ukuaji wa uchumi Nyamongo



Lori likiwa kazini katika 
mgodi wa Barrick North Mara.
--------------------------------------------

NA WAANDISHI WETU

---------------------------------


BAADA ya kukabidhiwa kwa Kampuni ya Barrick Gold, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umeendelea kuwa chachu na mhimili wa uchumi na maisha ya wafanyabiashara mbalimbali katika mji wa Nyamongo, wilayani Tarime.

Mzunguko wa fedha, majengo ya kisasa, huduma za kiuchumi kama vile vituo vya mafuta, hoteli na nyumba za kulala wageni, migahawa ya chakula, huduma za kusafisha magari na saluni za wanawake na wanaume vimeongezeka katika mji wa Nyamongo tangu Barrick ianze kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Inaelezwa kuwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa maisha ya wafanyabiashara na wakazi wa mji wa Nyamongo kwa ujumla unachangiwa kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi wa mgodi huo.

“Bila uwepo wa mgodi wa Barrick North Mara nisingekuwa hapa kufanya biashara hii ya kuuza chakula - kwa sababu wateja wangu wengi ni watu wanaofanya kazi katika mgodi huu,” anasema Justina Daniel - maarufu kwa jina la Mama Mdogo, mfanyabiashara ya mgahawa wa vyakula mjini Nyamongo.

Justina anabainisha kuwa miongoni mwa wateja hao wanatoka katika Idara ya Mahusiano ya Jamii ya Barrick North Mara na kampuni mbalimbali za wazawa zinazofanya kazi na mgodi huo.

“Ninaendelea vizuri na biashara yangu ya kuuza vyakula mbalimbali na bei ya hapa [mjini Nyamongo] ni kubwa kuliko hata Dar es Salaam,” anasema Justina katika mazungumzo na Sauti ya Mara mhagawani kwake hivi karibuni.

Anaongeza kuwa biashara hiyo imewavutia mabinti zake wiwili; Suzana na Neema Ryoba na tayari wameungana naye kuiendesha - wakisaidiana na wafanyakazi wanne waliowaajiri.

“Ninaona ninapiga hatua kimaendeleo kwa sababu faida ninayopata katika biashara hii inaniwezesha kupeleka watoto shule na kufanya maendeleo mengine katika familia. Ndoto yangu ni kumiliki mhagawa mkubwa siku zijazo,” anasema Justina.


Mfanyabiashara ya mgahawa wa chakula katika mji wa Nyamongo, Justina Daniel “Mama Mdogo” (kulia waliokaa), watoto na wafanyakazi wake wakifurahia jambo wakiwa kazini.
-----------------------------------------------

Afisa Mandeleo ataja
mageuzi makubwa
Kwa mujibu wa maafisa maendeleo ya jamii wa Serikali wanaofanya kazi katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara, mchango wa mgodi huo katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni mkubwa.

“Wazawa wa hapa wanapewa kipaumbele katika kutoa huduma kwenye mgodi wa Barrick North Mara, hivyo maendeleo ni mengi,” anasema Mary Kitesho Laizer, Afisa Maendeleo ya Jamii anayesimimia kata za Kemambo, Kibasuka na Nyarokoba zenye vijijiji vilivyo jirani na mgodi huo.

Mwanga zaidi kwa
kampuni za wazawa

Kuna uwezekano mkubwa kwa kampuni za wazawa zinazopata fursa za kibishara katika mgodi wa North Mara kuendelea kufanya vizuri zaidi baada ya kujengewa uwezo na Kampuni ya Barrick Gold.

Tayari kampuni 19 zimehitimu mafunzo ya miezi sita chini ya mpango wa uendelezaji wa biashara ulioanzishwa na Barrick North Mara kwa lengo la kuwajengea uwezo wafanyabiashara wazawa katika mkoa wa Mara.

Wamiliki wa kampuni hizo ni wafanyabishara wanaotoka maeneo yaliyo jirani na Mgodi huo.

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalilenga kuzifanya kampuni hizo kufanya biashara ndani na nje ya mgodi huo kwa ufanisi zaidi.

Mahafali ya kampuni hizo ya kuhitimu mafunzo hayo yalifanyika mgodini hapo mwezi uliopita, huku wamiliki na wawakilishi wa kampuni hizo wakiahidi kufanya mabadiliko makubwa katika biashara zao.

Marwa Robert kutoka Kampuni ya RAEOA Investment Limited anasema moja ya dosari ambazo wamejifunza kuwa zimekuwa zikifanywa na kampuni zinazopata fursa za kutoa huduma na kusambaza bidhaa ni kwenye mchakato wa ununuzi (quotation).

“Kwa mafunzo haya tutafanya vizuri zaidi, ulikuwa unakuta mtu ana- quote kitu cha kuuza shilingi elfu 10,000 anaweka bei ya juu kama shilingi 80,000 kwa kuwa ni Kampuni ya Barrick,” anaongeza Robert huku akiomba mafunzo hayo kuwa endelevu.

Wahitimu hao wanasema wameelewa pia umuhimu wa kulipa kodi serikalini kwa maendeleo ya Taifa - kutokana na mafunzo hayo.

“Suala la kulipa kodi lilikuwa changamoto lakini sasa tutakuwa mabalozi wazuri katika kuchangia mapato ya Serikali kwa kulipa kodi,” anaongeza Robert.

Pengine jambo jingine kubwa linaloweza kuzifanya kampuni hizo kukua na kupanua biashara zao ni kuacha sasa kutegemea mgodi huo peke yake, na kuanza kutafuta fursa za biashara nje ya mgodi huo.

“Sio tu kwamba tumejengewa uwezo wa kufanya biashara zetu vizuri na kwa ufanisi na mgodi wa Barrick, bali pia katika kufikiri nje ya ‘box’ kutafuta kazi nje ya mgodi wa Barrick,” anasema mmoja wa wahitimu hao.

Inaelezwa kuwa idadi ya kampuni za wazawa ambazo zinapata fursa ya kufanya biashara katika mgodi hiyo imeendelea kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

“Kuna ongezeko kubwa sana la kampuni za wazawa zinazofanya kazi na mgodi wa North Mara. Hilo ni jambo la kuipongeza sana Kampuni ya Barrick,” anasema Nicodemus Keraryo, mkazi wa Nyamongo na mmoja wa vijana wazawa wanaomiliki kampuni zinazofanya kazi na mgodi huo.

Anaongeza: “Mbali na Barrick ambao wanajitahidi sana kuwapa wazawa kipaumbele cha katika ajira mgodini, pia kwenye hizi kampuni za wazawa tumeajiri watu wengi kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi na kuwawezesha kupiga hatua mbalimbali za maendeleo.”

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na mgodi huo kuhakikisha kampuni za wazawa zinashiriki kikamilifu kutoa huduma na kusambaza bidhaa mbalimbali zinazohitajika mgodini.

“Kuhitimu kwa kampuni hizi ni alama muhimu katika kukuza biashara ya wazawa katika mkoa wetu wa Mara,” alisema GM Lyambiko.

Alibanisha kuwa mgodi wa Barrick North Mara umeendelea kuwapa wazabuni wazawa fursa ya kuhudumia na kusambaza bidhaa katika mgodi huo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.

Alitolea mfano wa Dola za Marekani milioni 37.4 sawa na takriban shilingi bilioni 95 ambazo zimelipwa na mgodi huo kwa wazabuni wazawa kwa mwaka 2023, huku ukitilia maanani falsafa ya ‘Local Content’.

Meneja Mkuu huyo alisema hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umesajili kampuni 118 ambazo zinapata fursa mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo.

Jambo la kufarahisha ni kwamba kampuni hizo za wazawa zimetoa ajira kwa watu 1,144, wengi wao wakiwa ni ambao wanatoka katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.

“Jitihada hizi sio tu zimechangia kwenye ustawi wa maendeleo ya jamii, bali zimesaidia katika kuimarisha mahusiano yetu na jamii inayotuzunguka,” alisema GM Lyambiko.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Tume ya Madini, Annasia Kwayu aliipongeza kampuni ya Barrick Gold na wahitimu hao, akisema mpango huo ni kielelezo halisi cha utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 na marekebisho yake.

“Tunatarajia huduma zote migodini ziwe bora na za kimataifa,” alisema Kwayu ambaye ni Meneja Ukaguzi wa Fedha, Kodi na Ushirikishwaji wa Watanzania kutoka Tume ya Madini.

Nguvu ya CSR kwenye
mzunguzuko wa fedha

Afisa Maendeleo ya Jamii, Mary, anasema mgodi huo umesaidia kuwezesha wakazi wa mji wa Nyamongo na maeneo mengine yaliyo jirani kuwa na uhakika wa kipato cha kujikimu na mahitaji mengine ya kimaendeleo.

Anaongeza kuwa hata mzunguko wa mabilioni ya fedha yanayotolewa na mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), umetengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi, wakiwemo wanawake.

Takwimu nyingine zinaonesha kuwa Kampuni ya Barrick kupitia mpango wake wa CSR, imetumia shilingi zaidi ya bilioni saba kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji mbalimbali kwa mwaka jana. Aidha, mwaka huu imetenga shilingi bilioni tisa kwa ajili ya miradi hiyo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini].

“Maendeleo katika mji wa Nyamongo ni makubwa sana, mfano kuna mpango wa kuwa na Shule ya English Medium (Mchepuo wa Kiingereza) ya Serikali kwa jamii ya hapa - ambayo wazazi wengi watamudu gharama.

“Lakini pia tumeshuhudia maendeleo ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari kutokana na fedha za CSR,” anaongeza Mary.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages