Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita na walimu wao katika Shule ya Sekondari Manga wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mahafali ya wanafunzi hao iliyofanyika shuleni hapo jana Aprili 16, 2024.
----------------------------------------------
Mara Online News, Tarime
------------------------------------
WANAFUNZI 135 wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Manga wilayani Tarime, Mara wameahidi kufanya vizuri zaidi katika mtihani wao wa kuhitimu, ili kuonesha mfano mzuri kwa wadogo zao shuleni hapo.
Walitoa ahadi hiyo mbele ya mgeni rasmi, walimu na wazazi wakati wa mahafali ya kidato cha sita ya nane, iliyofana kwa aina yake shuleni hapo jana Aprili 16, 2024.
“Tunaahidi ufauli wa daraja la kwanza na la pili tu katika mtihani wetu wa taifa utakaoanza Mei 6, mwaka huu. Tunaomba Mungu atupe afya njema, atulinde, atubariki na atufanikishe katika malengo yetu,” walisema wanafunzi hao kupitia risala yao kwa mgeni rasmi, iliyosomwa na Sarah Dedan na Swaumu hemed.
Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Manga akipokea cheti cha kuhitimu kutoka kwa mgeni rasmi, Mugini Jacob wakati wa mahafali hiyo.
------------------------------------------------
Kwa upande wake mgeni rasmi, Mugini Jacob ambaye ni Mkurugenzi wa Mara Online, aliwapongeza wanafunzi hao na kuwaombea mafanikio tele, lakini pia akiwahimiza kusoma kwa bidii, kujiamini na kudumisha nidhamu kwa walimu na wazazi wao.
“Tunawaombea mfanye vizuri zaidi katika masomo na mtihani wenu wa kuhitimu kidato cha sita ili kuwafurahisha walimu na wazazi wenu,” alisema Jacob ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa vyombo habari vya Mara Online News, Sauti ya Mara na Lake Zone Watch.
Mgeni rasmi Jacob (kushoto) na Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwl Editha Lazaro Nakei wakifuatilia jambo wakati wa mahafali hiyo.
------------------------------------------------
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwl Editha Lazaro Nakei, alisema wamewapatia wanafunzi hao elimu itakayowajengea msingi mzuri wa kufaulu ili kujiunga na elimu ya vyuo vikuu na vya kati.
“Pia elimu tuliyowapatia itawajengea uwezo mzuri wa kujitambua, kufikiri na kufanya maamuzi sahihi katika kazi za ujenzi wa taifa letu,” aliongeza Mwl Nakei.
Mwl Nakei akizungumza
wakati wa mahafali hiyo.
-------------------------------------------------
Aidha, Mwl Nakei alisema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 1,239 wa kidato cha kwanza hadi cha sita (wavulana 343 na wasichana 896), wafanyakazi wa kuajiriwa 32 wakiwemo walimu 25 na muuguzi, na walimu wa muda mfupi sita.
Mahafali hayo yalihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Manga, Sylvester Kisiri, Diwani wa Kata ya Manga, Leonce Baltazar, wakuu wa shule za sekondari mbalimbali na viongozi wa dini, miongoni mwa wengine.
Mwalimu Baraka Arkadi Krete akipokea zawadi ya shilingi zaidi ya laki nane kwenye bahasha iliyotolewa na uongozi wa Shule ya Sekondari Manga baada ya wanafunzi wengi kufaulu somo lake la Jiografia.
----------------------------------------------------
No comments:
Post a Comment