NEWS

Wednesday, 17 April 2024

Chandi ajivunia bilioni 600/- za maendeleo Mara, amwomba Kinana kumfikishia Rais Samia salamu za shukrani



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi akizungumza katika mkutano wa ndani wa wajumbe wa Halmashauri Kuu na mabaraza ya jumuiya za chama hicho wilayani Bunda jana.
-----------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Bunda
------------------------------------


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amemwomba Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana kumfikishia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan salamu za shukrani kwa kuendelea kuujali mkoa huo kimaendeleo.

“Nikushukuru sana Kinana kwa kuja mkoani Mara, tufikishie shukrani kwa Mama Samia, tunamshukuru kwa kuleta bilioni 600 [katika mwaka wa fedha 2023/2024], miradi mikubwa ya kimkakati imetekelezwa,” alisema Chandi wakati akimkaribisha Kinana kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mabaraza ya jumuiya za chama hicho katika mkutano wa ndani uliofanyika mjini Bunda jana.


Sehemu ya wajumbe mkutanoni.
-------------------------------------------

Chandi aliongeza: “Rais ameleta pikipiki (kwa viongozi wa kata) mfanye kazi, CCM tumejipanga, tulishasema diwani bora ni yule atakayehakikisha kwenye kata, kijiji, mtaa na kitongoji wagombea wetu wanashinda katika eneo lake la uongozi, fanyeni mikutano na kusimamia Ilani yetu vyema, ushindi wetu ndio unaotupa ridhaa ya kukaa madarakani.”

Kwa upande wake, Kinana aliwapongeza viongozi na wanachama wa CCM wilayani Bunda kwa kufanya kazi kwa ushirikiano.


Kinana akizungumza mkutanoni.
-------------------------------------------

“Hongera Bunda, mna majimbo matatu, wilaya moja na halmashauri mbili, hakuna mvurugano kama maeneo mengine niliyopita. Nimefurahishwa sana na mshikamano na ushirikiano hapa Bunda, Mama Samia anafanya kazi nzuri sana,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages