NEWS

Monday 29 April 2024

Mgodi wa Barrick North Mara wajenga shule ya kisasa Nyamongo



Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Matongo, Faustine Chacha Kikerero akionesha baadhi ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa na Barraick North Mara katika kijijini hapo.
------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
------------------------------------------


MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara upo mbioni kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi ya kisasa, ambayo huenda ikawa shule ya msingi bora ya serikali mkoani Mara.

Shule hiyo inajengwa katika kijiji cha Matongo, jirani na mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

“Kwa maana ya ubora wa miundombinu ya majengo, shule hii sio tu itakuwa bora katika wilaya yetu ya Tarime, bali hata mkoa mzima wa Mara na pengine hata kwa Tanzania,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe alisema katika mahojiano na Sauti ya Mara kijijini hapo juzi.

Tayari ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba 12 vya madarasa, jengo la utawala na vyoo vya kisasa kwa ajili ya wanafunzi umekamilika.

“Matamamio yetu ni kuona watoto wetu wanaanza kutumia shule hii mara baada ya likizo ya mwezi wa sita mwaka huu. Na tungetamani kuona pia Mwenge wa Uhuru mwaka huu unakesha hapa,” Itembe aliliambia gazeti hili.


Sehemu ya mbele ya jengo la utawala la shule mypa ya msingi Kenyangi inayojengwa na Barrick North Mara.
--------------------------------------------------

Mgodi wa Barrick North Mara umechukua hatua ya kujenga shule hiyo ili kuhamisha Shule ya Msingi Kenyangi yenye mamia ya wanafunzi kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi huo.

Uhamisho wa shule hiyo utakuwa na faida nyingi, kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Matango, Faustine Chacha Kikerero.

“Kuna utofauti mkubwa kati ya shule inayohamishwa na inayojengwa. Kwanza hatukuwa na jengo la utawala lakini mgodi umetujengea jengo zuri la utawala. Pili madarasa na miundombinu mingine ilikuwa imechakaa lakini sasa majengo yote yakiwemo madarasa ni mapya na yapo katika mpangilio mzuri unaovutia,” Kikerero anasema katika mahojiano na Sauti ya Mara ofisini kwake.

Anaongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo pia utasaidia kupaisha maendeleo ya kitaaluma katika shule hiyo.

“Kikubwa zaidi ujenzi wa shule hii utawapunguzia wanafunzi wengi umbali wa kutembea, na tunategemea ufaulu wa shule kuongezeka kutoka asilimia 75 kwa sasa hadi asilimia 100,” anasema Kikerero.

Ujenzi wa mradi huo wa shule unatekelezwa na wakandarasi wazawa ambao ni wafanyabiashara kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara.

“Huu ni mradi wa mfano na wakandarasi wetu wamefanya kazi nzuri sana, ni majengo yenye viwango mkubwa,” anasema Charles Ryoba, mmoja wa wakazi wa kijiji cha Matongo kilichopo jirani na mgodi huo.

Mgodi ni mdau mkubwa wa maendeleo
Wananchi na viongozi wa kijiji hicho wanauelezea Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kama mdau wao muhimu wa maendeleo.

“Barrick North Mara ni mdau mkubwa wa maendeleo katika jamii yetu na tunaendelea kumhitaji. Pia mahusiano yetu na mgodi kwa sasa ni mazuri,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Itembe, anahitimisha.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampui ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mgodi huo pia unaendelea kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR). Miradi inayopewa kipaumbele ni elimu, afya, usalama wa chakula, maji na uchumi.

Mahusiano kati ya mgodi huo na wananchi wanaoishi katika vijiji 11 vilivyo jirani nao kwa sasa yanaripotiwa kuimarika ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages