Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo (katikati) katika picha ya pamoja na wananchi wa kata ya Nyegina, wakiwemo walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bukwaya, Alhamisi iliyopita.
-------------------------------------------------
------------------------------------------
MBUNGE wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo amekabidhi saruji mifuko 150, iliyonunuliwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo hilo, kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari mpya ya Bukwaya.
Prof Muhongo alikabidhi saruji hiyo Alhamisi iliyopita, alipotembelea shule hiyo iliyopo kata ya Nyegina, Musoma Vijijini.
Wananchi wa kata ya Nyegina inayoundwa na vijiji vya Kurukerege, Mkirira na Nyegina walimshirikisha Mbunge Muhongo kufanya uamuzi wa kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya sekondari hiyo mpya iliyofunguliwa Julai 2022.
Walikubaliana kwamba ifikapo Aprili 30, 2024 vyumba viwili vya madarasa ambavyo tayari vimeezekwa viwe vimekamilika, na ifikapo Mei 30, 2024 matundu sita ya choo yawe yamekamilika.
Lakini pia ifikapo Julai 2024 Prof Muhongo ataongoza harambee ya kuanza ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi; ambayo ni fizikia, kemia na bailojia.
Shule ya Sekondari mpya ya Bukwaya ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na Mbunge Muhongo, kisha Serikali ikachangia ujenzi huo kwa shilingi milioni 40.
Shule hiyo inafanya kata ya Nyegina kuwa na shule mbili za sekondari. Nyingine ni Shule ya Sekondari Mkirira.
No comments:
Post a Comment