NEWS

Tuesday 2 April 2024

Waziri Mkuu Majaliwa akemea matumizi ya dawa za kulevya akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru 2024



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwasha Mwenge wa Uhuru kuzindua mbio zake mwaka huu katika sherehe zilizofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro leo Aprili 2, 2024.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Moshi
--------------------------------------


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu wa 2024, na kutumia nafasi hiyo kuwataka vijana kuacha matumizi ya dawa za kulevya, hasa bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi kiitwacho ‘Cha Arusha’ na Skanka.

“Vijana ambao mmekuwa mkitumia hiki ‘Cha Arusha’ na Skanka muache ili kunusuru maisha yenu. Vijana mnahitajika katika Taifa hili, vijana ndio mtakaolijenga Taifa hili, Vijana ndio muelekeo wa Taifa hili, ‘Cha Arusha’ na Skanka zitawapoteza kwenye muelekeo,” amesisitiza Majaliwa katika sherehe za uzinduzi huo ziliofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mkoani Kilimanjaro leo Aprili 2, 2024.


Waziri Mkuu Majaliwa akielekea kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa kiongozi wa mbio hizo kitaifa 2024, Godfrey Eliakim Mzava.
-----------------------------------------------

Majaliwa ambaye amemwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi kwenye sherehe hizo, amesema dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi zimeendelea kutumiwa kwa wingi nchini, na kwamba aina ya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi inayofahamika kama ‘Cha Arusha’ na Skanka ina sumu nyingi inayochanganywa kwenye sigara na kuwafanya watumiaji kubadilika na kuwa vichaa.

"Idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri wa miaka kati ya 13 na 24, kundi hili ni nguvukazi ya Taifa letu, Serikali haiwezi kunyamazi itaendelea kufanya msako mkali ili wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwe hatua kali," amesema.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema mbio za mwenge mwaka huu pia zitaendelea kusisitiza umuhimu wa kupambana na rushwa na maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii nchini.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 ni Godfrey Eliakim Mzava, na kaulimbiu ya mbio hizo mwaka huu inasema: “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages