NEWS

Tuesday 2 April 2024

Mmiliki wa mifugo 34 iliyouawa na chui Serengeti kufidiwa shilingi laki nane



Chui

NA MWANDISHI WETU, Serengeti
--------------------------------------------------


MKAZI wa kijiji cha Robanda na mmiliki wa mbuzi na kondoo 34 waliouawa na chui hivi karibuni anatarajiwa kulipwa shilingi lake nane kama kifuta jasho, mamlaka za serikali zimesema.

“Atajaza fomu kuanzia kijijini kwa kusaidiwa na viongozi wa kijiji ili malipo ya fidia yafanyike kwa njia ya kawaida,” Afisa Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan aliiambia Sauti ya Mara kwa njia ya simu wiki iliyopita.

Lendoyan alisema kwa mujibu wa kanuni zilizopo, kiasi cha fidia kwa mbuzi au kondoo mmoja ni shilingi 25,000.

Kwa hesabu hiyo, mmiliki husika atalipwa shiingi 850,000 kama kifuta jasho kutokana na mifugo yake 34 [mbuzi na kondoo] iliyouawa na chui.

Machi 16, mwaka huu chui alivamia banda la mifugo kijjini hapo na kuua mbuzi na kondoo 34, mali ya Mechakobo Ketenana.

Hata hivyo baada ya tukio hilo, maafisa wa wanyamapori wa serikali walimtega na kufanikiwa kumnasa chui huyo na kumhamishia maeneo ya uhifadhi.

Katika hatua nyingine, mamlaka za serikali zinamsaka chui mwingine anayehofiwa kuwepo katika kijiji cha Robanda, kabla hajafanya madhara kwa wananchi.

“Kuna chui mmoja ambaye tunamtafuta tumtoe kijijini Robanda, inasemekana yupo kijijini,” alisema Lendoyan.

Robanda ni miongoni mwa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti na mapori ya akiba ya Ikrongo-Grumeti katika ikolojia ya Serengeti mkoani Mara.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages