NEWS

Tuesday 30 April 2024

RC Mtambi aja na mikakati ya kutokomeza uvamizi mgodi wa Barrick North Mara kwa manufaa ya pande zoteMkuu wa Mkoa wa Mara, 
Kanali Evans Mtambi.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
---------------------------


MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema hafurahishwi na vitendo vya mauaji ya raia, uvamizi na wizi wa mawe ya dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

Kutokana na hali hiyo amebuni mikakati mahususi atakayoitekeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa matatizo hayo yanakomeshwa haraka iwezekanavyo.

“Binafsi nachukizwa na mauji ya raia, lakini pia kama kiongozi sipendi tabia za uvamizi zinazofanywa na vijana kuvamia mgodi, ndiyo maana kabla hata sijaapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, nilishaanza kutafakari namna ya kupata suluhisho la kudumu kwa matatizo haya,” RC Mtambi alimwambia mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu wiki iliyopita.

Alisema kwamba mara baada ya kuapishwa alianza kushirikisha mamlaka na wadau mbalimbali kukabiliana na matatizo hayo, ambapo pamoja na mambo mengine, hatua watakazochukua ni kuhakikisha kuwa kila upande unanufaika na suluhisho la matatizo hayo.

“Nikwambie tu kwa uhakika kwamba suluhisho hili nila uhakika na tumefikia hatua nzuri sana, ninashukuru kwamba mwitikio wetu ni mzuri mno.

“Ombi langu kwa vijana wa Tarime na jamii nzima kwa sasa ni kuwa watulivu ili watupe nafasi ya kutekeleza jambo hili kwa ukamilifu, wasifanye matukio ambayo yatahamisha umakini kuanza kushughulikia matatizo waliyoyasababisha badala ya kuwekeza nguvu kwenye kutekeleza mkakati huu ambao utakuwa ni win-win kwa pande zote,” alisema RC Mtambi.

Kiongozi huyo wa mkoa alisisitiza kuwa migogoro ya muda mrefu inayohusisha mgodi wa Barrick North Mara na wananchi wanaouvamia ili kuiba mawe ya dhahabu na kusababisha majeruhi na vifo utapatiwa suluhisho la kudumu kabla ya Julai mwaka huu.

Alisema moja kati ya mambo makubwa aliyokabidhiwa baada ya kuteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara hivi karibuni, ni pamoja na kutatua mgogoro huo ambao mbali na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu, umekuwa ukisababisha usumbufu na kukwaza uzalishaji katika mgodi huo.

RC Mtambi alisema mikakati yake itakuwa na hatua tatu za utekelezaji kuelekea kwenye suluhisho la kudumu.

Alifafanua kuwa katika hatua ya kwanza ameelekeza vyombo vya usalama, hasa Jeshi la Polisi kubadili mbinu za kushughulikia matatizo ya uvamizi mgodini, na katika hatua nyingine ameanza kuzifikia jamii zinazozunguka mgodi huo na kuzungumza nazo kutoa elimu.

Pia kuhamasisha makundi mbalimbali katika jamii ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari, wazee wa mila, viongozi wa dini, vijana na watu wenye ushawishi kuwaelimisha jamii, hasa vijana kuachana na uvamizi huo kwa kuwa serikali ya mkoa inachukua hatua kuelekea suluhisho ya kudumu.

“Hizi zote ni remedy (dawa) kutuliza tatizo hili linalokabili uhusiano wa jamii inayozunguka mgodi na mgodi wenyewe, lakini kama serikali tumeandaa mkakati wa kudumu kumaliza tatizo hili, na nikwambie mkakati huo uko pazuri, matatizo yote yanayokabili mgodi huu yatafikia ukomo ifikapo Julai mkwa huu 2024,” alisisitiza.

Mkuu huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi wa Tarime kumuunga mkono katika suala hilo kwa sababu lina manufaa kwa kila upande na kwamba vijana wa maeneo hayo wajiandae kunufaika na suluhisho hilo.

“Suluhisho hili limelenga kunufaisha kila upande kwa namna yake, vijana nawaomba wawe watulivu, siku si nyingi watakuwa matajiri, tunataka vijana wanufaike na mgodi ufanye kazi zake bila usumbufu,” RC Mtambi alisisitiza.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages