NEWS

Monday 29 April 2024

Maafa Kenya: Watu zaidi ya 40 wapoteza maisha baada ya bwawa kupasua kingo




MAKUMI ya watu wameuawa baada ya bwawa kupasuka kingo mapema leo Jumatatu katika eneo la Mai Mahiu nchini Kenya, kaskazini mwa mji mkuu, Nairobi, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limeithibitishia BBC.

Gavana wa eneo hilo, Susan Kihika pia amethibitisha vifo hivyo kwa shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Maji yalitiririka na kusomba nyumba na magari kadhaa katika kijiji cha Kamuchiri, kufuatia mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha maeneo kadhaa nchini Kenya.

Vikosi vya uokoaji vinachimba matope kutafuta manusura, vyombo vya habari vya eneo hilo vilisema, na kuonya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mvua hiyo ilipasua barabara kuu kutoka Nairobi kuelekea Mai Mahiu baada ya mawe makubwa, matope na magogo kuziba eneo hilo.



Mapema leo Jumatatu, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema limewapeleka watu kadhaa katika kituo cha afya huko Mai Mahiu kutokana na mafuriko.

Vifo vya watu zaidi ya 40 vilivyotokea leo vinafanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika maeneo mbalimbali nchini Kenya kutokana na mvua kubwa na mafuriko tangu mwezi uliopita kufikia zaidi ya 100.

Serikali yaanza ukaguzi wa mabwawa Kenya
Serikali ya Kenya imeagiza Kamati za Usalama na Ujasusi za Kaunti kote nchini kukagua mabwawa yote ya umma na ya binafsi kufikia kesho Jumanne.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki leo Jumatatu ameagiza kamati hizo kupendekeza baadaye kutolewa kwa amri za kuhamisha watu kwa lazima katika makazi ya watu yaliyo katika hatari hadi maeneo salama.

Hatua hiyo ni kufuatia kisa cha leo Jumatatu asubuhi ambapo bwawa limepasuka kingo huko Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru, na kusomba nyumba na magari, na kuua watu zaidi ya 40.



Mafuriko hayo yametoka kwenye mto ulio karibu ambao ulivunja kingo zake baada ya mvua kunyesha, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Waziri wa Mambo ya Ndani aliagiza kaunti kupeleka vikosi vya kutekeleza sheria katika maeneo ya barabarani ambayo hukabiliwa na mafuriko na na katika sehemu zadaraja ili kuzuia madereva au watembea kwa miguu kuhatarisha maisha yao kwa kuvuka.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages