NEWS

Friday 26 April 2024

Shirika la Ndege Kenya laishutumu DR Congo kuwazuia wafanyakazi wake




SHIRIKA la Ndege la Kenya (KQ) limelishutumu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) kuwashikilia wafanyakazi wake wawili tangu wiki iliyopita, licha ya mahakama kuamua waachiwe huru.

Wawili hao walikamatwa na kitengo cha kijasusi cha kijeshi cha DR Congo Ijumaa iliyopita kwa madai ya kutokuwa na nyaraka za forodha kwenye shehena ya "thamani," KQ ilisema katika taarifa.

Shirika hilo la ndege lilisema halikusafirisha mizigo hadi Kinshasa kutokana na kutokamilika kwa nyaraka.

"Juhudi zote za kuwaeleza maafisa wa kijeshi kwamba KQ haikukubali shehena hiyo kwa sababu ya kutokamilika kwa nyaraka ziliambulia patupu," iliongeza.

Maafisa hao wa kijeshi waliwazuia wafanyakazi hao wawili wa KQ hadi Jumanne, wakati maafisa wa ubalozi wa Kenya na timu ya shirika la ndege waliporuhusiwa kuwatembelea kwa muda mfupi.

Alhamisi, KQ ilisema mahakama ya kijeshi ilikubali ombi lake la kutaka wafanyakazi hao waachiwe huku uchunguzi ukiendelea.

"Licha ya maagizo ya mahakama, kitengo cha kijasusi cha kijeshi bado kinawashikilia kwa siri, lakini hawa ni raia wanaozuiwa katika kituo cha kijasusi cha kijeshi," shirika hilo la ndege liliongeza.

Simu za wafanyakazi hao zilichukuliwa wakati wa kukamatwa kwao, kulingana na KQ.

Haijulikani ni shehena gani iliyotajwa na mamlaka nchini DR Congo kwani bado hazijazungumzia suala hilo.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages