NEWS

Friday 26 April 2024

Mugumu: Wenyeviti wa vitongoji wailalamikia Halmashauri ya Serengeti kutowalipa mamilioni ya fedha za posho zao



Sehemu ya mji wa Mugumu 
wilayani Serengeti, Mara.
-----------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa/
Mara Online News
---------------------------


WENYEVITI 30 wa vitongoji vinavyounda Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu wameibana Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wakitaka iwalipe malimbikizo ya posho zao za vikao na madaraka - kiasi cha shilingi milioni 26.

Malimbikizo hayo ni ya kuanzia mwaka 2019 hadi 2024, kwa mujibu wa wenyeviti hao.

Walilalamika kucheleweshewa posho hizo wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo hivi karibuni.

“Watulipe posho zetu ni haki zetu za msingi sio hisani,” alisema Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamerama, Mwita Marwa Nyanswi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Bwenda Ismail Bainga alikiri kuwepo kwa madai ya posho za wenyeviti hao.

“Haya ni madeni tuliyoridhi kutoka utawala wa nyuma (wakurugenzi waliopita) kuanzia mwaka 2019, tumeyapokea na tutayalipa yote kwa awamu. Hizi ni fedha za serikali, kuanzia sasa tunaendelea kutazama nyaraka tupate yaliyo sahihi yalipwe,” Bainga aliiambia Mara Online News kwa njia ya simu.

Naye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu, Charles Chacha Ally alikiri kuwepo kwa ahadi ya ulipaji wa posho hizo.

“Ni kweli wameahidi kulipa deni hilo kidogo kidogo kutokana na vyanzo vya halmashauri, japo hiyo sio mara ya kwanza kutuahidi, walishaahidi zaidi ya mara sita. Naomba watulipe ni fedha zinazofahamika kikanuni na kisheria maana zinatusaidia kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages