NEWS

Friday 26 April 2024

Mwenyekiti CCM Simiyu amvaa vikali Mpina kifo cha Magufuli



Shemsa Seif Mohamed
-------------------------------


Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shemsa Seif Mohamed amemshukia Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani humo, Luhaga Mpina, akimtaka kuacha alichokiita siasa za maji taka za kuhoji sababu za kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe Joseph Magufuli na kuchafua viongozi wa kitaifa.

“Wabunge wangu wa mkoa wa Simiyu wakafanye yale wananchi waliyowatuma, waachane na siasa za maji taka - za kuchafua ziongozi wa kitaifa.

“Badala ya kuhangaika na matatizo ya wananchi wa jimbo lake anahangaika kutafuta sababu ya kifo cha Magufuli. Wana-Kisesa wanasikitika sana kwa sababu yale waliyomtuma haendi kuyatekeleza,” amesema mwenyekiti huyo.

Shemsa alitoa kauli hiyo jana Aprili 25, 2024 wakati wa ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa mkoani Simiyu, iliyofanyika katika tarafa ya Kanadi wilayani Itilima, ikiwa ni sehemu ya kukagua na kuimarisha uhai wa CCM kwa kukutana na mabalozi, viongozi wa matawi, mashina na madiwani.

Aliendelea: “Nimetoka jimbo la Kisesa wananchi wanalia kwa sababu wana changamoto nyingi, mbunge wao haonekani, toka wamemchagua miaka mitano - sehemu zingine hajawahi kufika - kukanyaga, mtafute mbunge yuko wapi - yuko anahangaika na kifo cha Magufuli.”

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Simiyu alitumia nafasi hiyo pia kumshauri Mpina kujikita katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowajima maendeleo wakazi wa jimbo la Kisesa badala ya kuhoji kifo cha mtu aliyetangulia “mbele ya haki”.

“Arudi jimboni akatatue kero za wananchi… wananchi wake wanateseka na tembo, aende akapambane na Waziri wa Maliasili, wananchi waache kuteseka. Asiende kupambana na mipango ya Mwenyezi Mungu anapochukua watu wake.

“Ulipewa uwaziri, kipi kizuri ulichokifanya wewe kuanzia kwenye ukoo - kwenye wilaya yako husika, ni mbunge anayeongoza hata kwa kutoshiriki vikao vya chama,” alisema Shemsa na kuhoji: “Unakwenda kuhoji bungeni kifo cha mtu aliyetangulia mbele za haki, ndicho wananchi walichokutuma?”


Kuhaga Mpina
---------------------
-


Hivi karibuni, Mbunge Mpina alinukuliwa na kuripotiwa na vyombo vya habari akiwasilisha hoja bungeni ya kutaka iundwe tume huru itakayochunguza alichokiita utata wa kifo cha Rais Dkt Magufuli.

“…kutokutolewa taarifa kamili kuhusu kifo cha Magufuli… nimeshawishika na ninawashawishi wabunge wenzangu kuruhusu kuunda tume huru ya kuchunguza utata wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe Joseph Magufuli ili kumtendea haki Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli, lakini na watu wengi waliotajwa aidha kwa wema au kwa ubaya katika suala hili.

Mpina ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu kupitia chama tawala - CCM, aliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi mwaka 2017 hadi 2020 katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages